33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Waganga wa jadi wapigwa marufuku kutoa tiba gesti

NA RAYMOND MINJA- IRINGA

MWENYEKITI wa Shirikisho la Vyama vya Tiba Asilia Taifa (SHIVIWATA), Abdulraman Lutenga, amepiga marufuku waganga wote wa jadi nchini kutoa huduma za tiba katika nyumba za kulala wageni.

Marufuku hiyo imekuja baada ya malalamiko ya muda mrefu ya wateja wanaokwenda kupata huduma katika maeneo hayo, hasa wanawake, kwamba wamekuwa wakifanyiwa na waganga hao vitendo vya udhalilishaji ikiwemo ubakaji.

Akizungumza katika kikao cha pamoja kilicholihusisha Jeshi la  Polisi Mkoa wa Iringa na waganga hao kutoka mkoani hapa, Lutenga alisema kuanzia sasa yeyote atakayekutwa anatoa huduma katika nyumba za kulala wageni atachukuliwa hatua  kali za kisheria.

Alisema kuwa sheria zao zinamtaka mganga wa tiba asilia kuwa na sehemu yake maalumu ya kufanya kazi hiyo na sio katika nyumba za kulala wageni na barabarani kwani wataalamu wengine ambao si waaminifu hutumia mwanya huo kuwafanyia vitendo viovu wateja wao.

 “Ndugu zangu hii sio masihara na hatuna utani, ni marufuku kufanyia huduma kwenye gesti, wengi wamekuwa wakiwabaka akina mama na wasichana wanaoenda kupata tiba kwa kisingizio cha kumtibu, hii sio sawa. Kuanzia leo ni marufuku na atakayekamatwa leseni yake tutaifungia,” alisema.

Mbali na marufuku hiyo, pia Lutenga alisema kuwa kuanzia sasa hakuna mganga yeyote atakayeruhusiwa kupiga ramli kwani wengi wao hupiga ramli chonganishi ambazo husababisha kutokea mauaji au kugombanisha jamii.

Alisema kuwa ramli nyingine hupigwa na kuwaambia watu wakawaue mama zao au watoto wao ili wapate mali jambo ambalo si sahihi kwani hakuna utajiri wa kumtoa mtu kafara bali hizo ni imani potofu.

Kwa upande wake Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Iringa, ASP Issa Sulemani, aliwataka waganga hao kufanya kazi yao bila ya kutenda uhalifu kwani endapo watafanya hivyo sheria haitasita kuwashughulikia.

Alisema kuwa kumekuwa na waganga wa tiba asilia wanaofanya kazi zao kwa kutenda uhalifu kwa kuwatuma wateja wao kwenda kutekeleza

mauaji au kuleta baadhi ya viungo vya binadamu ili kujipatia mali, kitu ambacho ni kinyume na sheria za nchi.

 “Ndugu zangu kila mtu afanye kazi kwa kufuata sheria, achaneni na hii tabia ya kutuma watu viungo vya watoto au unamtuma mtu akatembee na mama yake, tabia ya wapi, nasema acheni ili twende sawa, la sivyo sheria itachukua mkondo wake,” alisema.

Aliwataka waganga wa tiba asilia hasa wanaume kuachana na tabia ya kuwabaka na kuwadhalilisha wanawake pindi wanapowapa matibabu.

“Tabia hii imeshamiri sana kwa waganga wa kiume, kwani hatujawahi kusikia kuwa mganga wa kike kambaka mteja wake wa kiume,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles