27.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

‘Waganga tuitwe, tushirikishwe vita dhidi ya chanjo’

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

KUTOKANA na ushawishi mkubwa walionao kwenye jamii, Serikali inapaswa kuwashirikisha waganga wa kienyeji kwenye programu za kusambaza elimu juu ya chanjo ya Corona.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Shirikisho la Waganga wa Kienyeji mkoani Simiyu, Mayunga Juma Kidoyayi, aliyedai kuwa waganga wana nafasi kubwa kutokana na imani kubwa waliyonayo Watanzania juu yao.

“Asilimia kubwa ya wananchi huwa wanakwenda kwa waganga na imani yao ni kubwa sana kwetu. Nikwambie tu, mganga anaweza kutumia maneno machache kukubalika, ukilinganisha na mtu mwingine,” amesema Kidoyayi.

Kwa upande mwingine, Kidoyayi anayekiri kupata chanjo ya Corona, amesema si jambo geni kwenye historia kwani hata zamani zilikuwapo, licha ya kwamba jamii ziliendelea na tiba za asili.

“Inawezekana ukawa unatumia njia zako asili kama vile kupiga nyungu, pia ukachanjwa. Mfano mzuri ni mimi, nimetumia dawa zangu lakini nimeshapata chanjo ya Corona,” amesisitiza.

Wakati Kidoyayi akihimiza hilo, Mganga wa Tiba Asili katika eneo la Mtoni Kijichi jijini Dar es Salaam, Shabani Msemakweli, anasema magonjwa aina ya Corona yalianza zamani.

“Kama ni tiba, tunapambana nayo na wagonjwa wanakuja. Tunawaangalia kama mtu ana dalili zinazotajwa, kama tunaweza kuzitatua basi tunazitatua. Jambo la msingi ni kuamini kuwa ugonjwa upo na jamii inapaswa kuupokea na kufuata utaratibu wa chanjo uliowekwa na Serikali,” anasema Msemakweli.

Kwa upande wake, Bonventura Mwalongo ni Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asili na Ulinzi wa Mazingira akiwa pia ni Mtaalamu wa Tiba Asili, anasema mtazamo wao kuhusu changamoto ya Corona ni kuona juhudi za pamoja zikifanywa, ikiwamo kuimarisha tafiti za dawa.

“Pamoja na chanjo, lakini kwanza tunahitaji kuendelea kuimarisha tafiti zinazohusu dawa za kutibu changamoto au dalili zote zinazoambatana na Corona, ikiwa ni pamoja na kutumia dawa zote za asili zilizothibitika kuwa na uwezo wa kutibu ugonjwa huu,” anasisitiza.

Bonventura Mwalongo, Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asili na Ulinzi wa Mazingira akiwa pia ni Mtaalamu wa Tiba Asili.

Aidha, Mwalongo anagusia umuhimu wa kuwapo kwa mtandao mzuri wa upatikanaji wa vituo vyote vya kutolea huduma za afya, ikiwa na maana kwamba kila hospitali pawepo na dirisha la dawa asili na muhudumu wake.

“Mfano, kwa Dar es Salaam pale Magomeni Kagera kuna duka la dawa asili la Boresha, hivyo ifike mahala dawa hizi za asili kutoka kwa wataalamu waliosajiliwa zipatikane kirahisi,” anasema Mwalongo.

Wakati huo huo, Mwalongo ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Pamoja ya Wizara ya Afya na Wadau wa Tiba asili, anasema ili kuweza kulikabili janga la Corona, inapaswa makundi yote kuja pamoja kwa maana ya tiba asili na yale ya tiba ya kisasa.

“Kama tunavyojua, kwamba kuna eneo la tiba asili na kuna lile la tiba ya sayansi ya kisasa kwani pamoja na tiba asili kuonekana kutokuwa mbadala wa chanjo, lakini bado zinapaswa kutumika kwa kuzingatia miongozo na maelekezo ya wataalamu na Serikali ili kila mwenye kuzihitaji aweze kuvitumia kama Rais Samia Suluhu alivyosema kuwa chanjo hizi ni hiari.

“Lakini pia, kama unaona bado hujapata Corona au umepata na unahitaji kupata chanjo kwa ajili ya kinga, basi chanja na ufanye hivyo kwa hiari yako bila kuona kama kuna mtu anakushurutisha kulinda afya yako,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mwalongo ametoa wito kwa Watanzania kushirikiana katika tafiti, taarifa na kuchukua hatua za kuzikinga jamii zao dhidi ya maradhi yatokanayo na wanyama, ndege au wadudu.

Ashura Njaidi anasema kuna umuhimu kwa wataalamu hao wa tiba asili kuhususishwa kwenye utaratibu huo wa kukabiliana na janga la corona kwani dawa nyingi zinatokana miti na mimea.

“Ni wazi kabisa kwamba dawa nyingi zinatokana na mimea asili ikiwemo miti, hivyo hata mjwenye mapambano haya pamoja na kwamba tumepata chanjo ya corona lakini nivyema pia kwa kundi hili muhimu kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya corona,”anasema Ashura ambaye ni mkazi wa Tandale jijini Dar es Salaam.

Wakati Ashura akisema hayo, upande wake, Anna Matingwa mkazi wa Dar es Salaam anasema kuwa binafsi amekuwa akitumia tiba asili na kwamba madhara yake yamekuwa ni machache.

“Unajua hata zama za mababu zetu walikuwa wakitumia tiba asili kwa jili ya kujitibia na maradhi mbalimbali kwani athari zake zimekuwa ni ndogo ikiwamo kutokuwa na kemikali, hivyo pamoja na kwamba chanjo imepatikana lakini ni busara zaidi kuwa na ushirikishwaji kwa makundi mbalimbali yaliyoko kwenye eneo hili la tiba,”amesema Anna.

Mwisho, Watanzania mbalimbali wanaendelea na uchanjaji wa chanjo ya Corona kwenye vituo zaidi ya 550 nchini kote, ambapo kwa mujibu wa Wizara ya Afya, zoezi hilo linaenda vizuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles