BRASILIA, BRAZIL
MAOFISA wa usalama nchini Brazil wamesema wafungwa wasiopungua 60 wameuawa katika ghasia zilizozuka katika gereza moja Kaskazini Magharibi mwa nchi.
Taarifa zinasema kuwa wengi wa waathirika wamekatwa vichwa.
Vurugu hizo zililipuka Jumapili katika gereza la Anisio Jobim mjini Manaus, baada ya magenge hasimu ya wafungwa kuanza kushambuliana.
Katika gereza jingine lililo umbali wa kilomita 100 kutoka Manaus, wafungwa 87 walifanikiwa kutoroka, lakini maofisa waliweza kuzima uasi mwingine katika gereza la tatu lililo karibu na hilo.
Ofisa wa usalama katika Jimbo la Amazonas yaliko magereza hayo, Sergio Fontes ameviambia vyombo vya habari kuwa ghasia hizo zilizodumu kwa muda wa saa 17 zilisababishwa na magenge yanayouza dawa za kulevya magerezani.
Huu ndio uasi mkubwa magerezani nchini Brazil tangu mwaka 1992 wakati wafungwa 111 walipouawa kwenye vurugu zilizotokea gereza la Carandiru mjini Sao Paolo.