23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

AFRIKA ITEGEMEE NINI KUTOKA KWA RAIS DONALD TRUMP?

Na BALINAGWE MWAMBUNGU


donald-trumpKAMA viongozi wa nchi za Kiafrika walikuwa na matumaini kwamba Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump, atakuwa mkarimu kwao kwa maana ya kuendelea kuwapa msaada katika nyanja mbalimbali kama walivyokuwa wanafanya watangulizi wake, wasahau kwa sababu yeye kipaumbele chake ni kuiona Marekani inachukua nafasi yake kama taifa kubwa lenye nguvu duniani.

Lakini mbaya zaidi, ni ule mtazamo wake kuhusu majimbo katika baadhi ya nchi za Kiafrika ambayo yanataka kujitenga; anasema wananchi wa majimbo hayo, wana haki ya kudai kujitenga, kwa kuwa ni sehemu ya demokrasia. Trump alinukuliwa na vyombo vya habari akisema:

“Kama watu wa Afrika wanataka uhuru, chini ya utawala wangu watapata wanachokitaka kupitia kura ya maoni. Kura ya maoni ni kitendo cha kidemokrasia, Waafrika wanayo haki ya kuendesha kura ya maoni.”

Aidha, Trump ameweka wazi kwamba hatawavumilia watawala waovu na wababe wanaovunja misingi ya demokrasia kwa kuendelea kutawala kama wafalme huku wakifuja rasilimali za nchi zao. Amesema asingependa kuwaona viongozi hao wakitembeza bakuli kwenda Marekani kuomba misaada.

 

Matamshi kama hayo, yanaashiria nini kwa Afrika? Nchi nyingi za Kiafrika zimekuwa na migogoro ya ndani kutokana na baadhi ya majimbo katika nchi hizo kutaka kujitenga, lakini hayakufanikiwa. Hii ni kwa sababu Serikali za sasa zimetumia nguvu kuwanyamazisha wananchi ambao wanaona ni haki yao kusimama kama nchi.

Mwaka 1967, jimbo lililokuwa linaitwa Nigeria Mashariki, lilitangaza kujitenga kutoka Serikali ya Shirikisho la Nigeria na kujiita Biafra.

Chini ya uongozi wa Luteni Kanali Chukuemeka Odumegwu Ojukwu, kabila la Waibo, ambalo ni la pili kutoka Wahausa, kwa ukubwa, walidai kuwa walikuwa wanabaguliwa, wanapuuzwa na waliokuwa wanaishi nje ya Biafra, hasa Kaskazini mwa Nigeria, walikuwa wanauawa na kunyang’anywa mali zao na Serikali ya Shirikisho la Serikali ya Nigeria, ilikuwa haichukui hatua za kudhibiti mauaji na kuwalinda wananchi wake.

Kitendo cha Kanali Ojukwu kuitangazia dunia kwamba Biafra sasa ilikuwa nchi huru, kiliifanya Serikali ya Shirikisho la Nigeria itangaze vita dhidi ya uasi wa Biafra, vita ambayo ilianza 1967 hadi 1970.

Marais wengi wa Kiafrika wanayo sababu ya kuogopa kwa kuwa nchi zao zina migogoro ya ndani, kuna baadhi ya majimbo hayaoni kama ni sehemu ya nchi hizo kwa kuwa yaliunganishwa kwa nguvu na wakoloni. Majimbo kama kwa Zulu-Natal (Afrika Kusini), kwa miaka mingi, wakati wa mapambano dhidi ya utawala wa Makaburu, liliendesha Serikali yake ya jimbo chini ya utawala wa kimila ukiongozwa na Chifu Mongosuthu Buthelezi.

Harakati hizo zilikoma mara tu baada ya Nelson Mandela kuachiwa kuru kutoka Kisiwa cha Robben na chama cha African National Congress (ANC) na vyama vingine kukubaliana kuunda Serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa. Baada ya uchaguzi mkuu wa kwanza, Buthelezi alishirikishwa katika Serikali iliyokuwa inaongozwa na Rais Mandela.

Kwa Afrika inaelekea Rais Donald Trump ataleta changamoto ambazo, bara hili lilianza kuzisahau changamoto za majimbo kama vile Katanga, nchini DRC. Katanga, jimbo tajiri sana kwa madini, liliwahi kujitangazia uhuru kutoka nchi iliyokuwa inaitwa Congo, ambapo iliongozwa kwa muda mfupi na Rais Joseph Kasavubu na Waziri Mkuu wa kwanza, Patrice Lumumba ambaye aliuawa na vikosi vya Ubelgiji kwa kushirikiana na majasusi wa Kimarekani. Tangu wakati huo, Congo ni kama ililaaniwa. Hivi sasa kuna vikundi vingi vya kikanda, kikabila vinavyotaka kujitenga na DRC.

Aidha, Marekani na nchi nyingine za Magharibi zilishiriki kuhakikisha kwamba Sudan Kusini inajitenga na Serikali ya Khartoum. Trump anaweza kuwa mwiba kwa Rais wa hivi sasa wa Sudan, Omar Al Bashir ambaye Serikali yake inapigana na waasi wa Darfur.

Nchi nyingine ambayo inaweza kukosa utulivu kutokana na siasa za Rais Trump ni Senegal.

Kwa muda mrefu imekuwa na mgogoro wa kisiasa na jimbo la Casamance, ingawaje uhasama huo ulimalizwa kwa mazungumzo mapema mwaka 2014.

Ethiopia, pamoja na kwamba nchi za Magharibi zimewekeza kwa wingi, lakini haitarajiwi kwamba Rais Trump ataweza kuwaunga mkono wananchi wa Oromo ambao wanataka kushiriki zaidi katika utawala wa Addis Ababa.

Nchi ya Angola iliendesha vita ya muda mrefu na kikundi cha waasi kutoka jimbo tajiri kwa mafuta la Cabinda na Trump anapotamka kwamba ataunga mkono juhudi za majimbo yanayotaka kujinasua kutoka Serikali kuu, atakuwa anafufua ndoto za watu wenye uroho wa madaraka.

Ikumbukwe kwamba, Nigeria pia imepita katika msukosuko mwingine wa watu wa Rivers State na Delta ambao wanadai utajiri wao wa mafuta hauwasaidii na Ken Saro-Wiwa, mwanaharakati aliyekuwa anaongoza wananchi kudai haki zao aliuawa na utawala wa Sani Abacha.

Majirani zetu Kenya nadhani nao hawatalipokea vizuri jambo hili. Tayari kule Pwani kuna kikundi kinachojiita Mombasa Republican Council, ambacho kimsingi kinataka watu waliotoka bara warudi kwao kwa sababu wameshika ardhi yote nono ya Pwani na wanachukua nafasi nyingi katika kazi.

Wakati wa kampeni, mara nyingi alisisitiza kauli mbiu yake ya kuifanya Marekani taifa kubwa na lenye nguvu, Make America-Great Again. Trump anawatia hofu viongozi wa Kiafrika ambao wanaendesha nchi zao kama mashamba yao binafsi.

Marekani katika historia yake ya kibabe, iliweza kujitanua na kushamiri katika maeneo ambayo kulikuwa na vikundi vilivyokuwa vinapinga tawala za mabavu, kwenye nchi kadhaa Amerika ya Kusini, Kusini Mashariki mwa Asia, Viet Nam na Cambodia, ilikuwa swahiba wa karibu na utawala wa kibaguzi wa Makaburu wa Afrika Kusini na ilimsaidia kilojistiki haini Jonas Zavimbi wa Angola na kumuunga mkono Jenerali Joseph Mobutu wa Zaire.

Afrika itamkumbuka Rais Barack Obama kwa vile si tu kwa sababu ya asili yake ya Afrika, lakini aliendeleza mazuri yote aliyoyafanya Rais George W. Bush (Republican), ambaye alitoa fedha nyingi sana kwa ajili ya mpango wa kupambana na Ukimwi, kusaidia mipango ya elimu na alianzisha Mfungo Maalumu wa Maendeleo ujulikanao kama Millennium Challenge Corporation.

Mara baada ya kuchaguliwa, mahasimu wa Trump walisema kuwa Wamarekani wameamua kurudi kinyumenyume kwa maana ya kwamba Rais huyo ni bepari na mhafidhina. Katika kampeni alisema atafuta programu zote za Rais Obama ambazo anadai zina harufu ya ujamaa. Kwa hiyo Afrika, kwa muda wa miaka minne ya utawala wa Trump, isitegemee kwamba utakuwa ni utawala rafiki na wenye msaada kwa bara hili.

Trump amesema ataitazama upya mikataba yote ya kibiashara na nchi zote, si tu za Kiafrika, bali hata Ulaya, Amerika ya Kusini na Asia na mikataba ambayo utawala wake utaona hauifaidishi Marekani, ataufuta au kufanya majadiliano upya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles