Na ATHUMANI MOHAMED
IMEKUWA kawaida katika familia zetu, mtu fulani kwenye ukoo akiwa na haueni ya maisha au akipata fursa ya kuishi mjini, basi ndugu zake hupenda kwenda mjini kumtembelea.
Si jambo baya kwa hakika, maana huzidisha upendo kwa familia na kujenga mshikamano. Kutembelewa na ndugu ni baraka. Lakini leo nataka nizungumzie kuhusu ndugu zetu ambao hualika ndugu zao wengi nyumbani na kufikia kukaa bila kazi maalumu.
Lakini pia upande wa pili ni kwa wale wenye tabia za kufunga safari na kwenda mjini kwa ndugu, kisha akifika huishia kusema, “Nimekuja kupumzikapumzika kidogo.”
Ukitazama kwa juujuu unaweza kuona siyo tatizo, lakini ukija katika mtazamo wa kutazama mambo kwa jicho la kimaisha, utagundua kuwa utakuwa unaishia kusifiwa kuwa una roho nzuri lakini kumbe unafanya mambo ambayo yapo juu ya uwezo wako.
Siku za hivi karibuni, wapo watu ambao wamekuwa na ufahamu wa hizi habari, wamekuwa hawataki kusikia kabisa habari za watu kurundikana nyumbani bila shughuli maalumu.
WAGENI NYUMBANI
Kama nilivyotangulia kueleza hapo juu, kutembelewa na wageni ni jambo la baraka. Si kitu kibaya kwa hakika, lakini lazima kuwe na utaratibu. Maisha ya mjini yana changamoto nyingi, yanahitaji hesabu za hali ya juu ili uweze kufanikiwa na kupiga hatua siku hadi siku.
Haiwezekani ukawa unafanya kazi kila siku fedha zinaishia kweye matumizi ya mlo tu. Kama ni kutembelewa, kwa kawaida mgeni anayetoka mkoani, anaweza kukaa nyumbani si zaidi ya mwezi mmoja (kipindi kirefu zaidi), tena huyu awe amefika kwa ajili ya likizo au jambo fulani maalumu.
Muda unaokubalika zaidi ni angalau wiki mbili, tena mwenyeji awe na taarifa mapema juu ya ujio wa mgeni huyo ili ajue namna gani ya kujipanga kumuhudumia katika muda ambao mgeni huyo atakuwa nyumbani hapo.
Lakini kama ni mgonjwa, amefika kwa ajili ya matibabu, hilo ni shauri jingine. Huyu hana muda maalumu wa kukaa hapo, kutegemeana na kushughulikia afya yake.
WANAKUSAIDIA?
Sina maana kwamba ni vibaya ndugu kuishi na ndugu zake mjini, lakini cha msingi wana kitu gani cha kufanya? Ni sahihi zaidi, ikiwa kama watajishughulisha kwa kazi ndogondogo za nyumbani ambazo zitaingiza angalau kipato.
Mfano, kuliko kukaa nyumbani bure ni afadhali afunge barafu au ice cream auze kuliko kukaa siku nzima akiangalia runinga sebuleni. Kukaa na ndugu ambaye hafanyi chochote ni afadhali uonekane una roho mbaya kwa kumrudisha nyumbani.
HUU NDIYO UKWELI
Wengi hawasemi tu, lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu anayependa kuishi na ndugu nyumbani kwake ambao hawana kitu cha kufanya. Watabaki wananung’unika au kutafuta visa na kuwafanya waondoke wenyewe na kusababisha mgongano kwenye familia, lakini hawatasema ukweli.
Dawa nzuri zaidi ni ukweli. Kwanza mwonyeshe namna ya kufanya ili awe na shughuli yake, kama hataki arudi kijijini. Lakini pia lazima ufanye mambo yako kwa uwazi; potelea mbali hata kama utaonekana una roho mbaya, ndugu yako akitaka kuja au akija, lazima umwulize atakaa siku ngapi.
Awe wazi kwa hilo, vinginevyo aeleze mipango yake kwa muda wote atakaokaa kwako. Si vizuri kuwa mnafiki, ni afadhali uonekane una roho mbaya kuliko kutafutia watu sababu ambazo si za maana.
Lakini la muhimu zaidi ni bora kumfundisha kutafuta, kuliko kumpa bure kila siku, maana mwisho wake atalemaa badala ya kujifunza kutoka kwako.