AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAMÂ
WATU watatu wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam kwa mashtaka mawili ikiwamo kula njama na kutenda kosa la wizi.
Waliofikishwa kortini ni Sabina Mushi (28) mkazi wa Sinza Makaburini, Dotto Silver (45) mkazi wa Manzese na Abdul Zemba (27) mkazi wa Tandale.
Akisoma shtaka la kwanza mbele ya Hakimu Joyce Mushi, Mwendesha Mashtaka, Abudi Yusuph, alidai kati ya Desemba 27 na 29 mwaka jana katika Mkoa wa Dar es Salaam, washtakiwa kwa pamoja walikula njama kutenda kosa la wizi.
Katika shtaka la pili ilidaiwa Desemba 29 mwaka jana, eneo la Makumbusho Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa waliiba kompyuta mpakato ya Dell yenye thamani ya Sh 3,000,000, simu moja ya Tecno yenye thamani ya Sh 300,000, vifaa vya jikoni yenye thamani ya Sh 75,000, ndoo ya sabuni ya Foma yenye thamani ya Sh 14,000 na vyeti mbalimbali vya taaluma vyote vikiwa na thamani ya Sh 3,389,000, mali ya Privatus Lipili.
Washtakiwa walikana mashitaka na walirudishwa rumande mpaka kesi hiyo itakapotajwa tena Machi 28 mwaka huu.
Wakati huo huo, Asteria Charles (31) ambaye ni muhudumu wa nyumba za wageni na mkazi wa Kigogo Luhanga, alipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa shtaka la kukutwa na noti mbili za bandia za Sh 10,000.
Mwendesha Mashtaka, Matarasa Hamisi, alidai mbele ya Hakimu Anifa Mwingira kuwa Novemba 19 mwaka jana eneo la Kigogo Wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa alikutwa na noti bandia zenye namba BT. 8356324 na BT. 8356326.
Mshtakiwa alikana shitaka na alirudishwa rumande hadi kesi yake itakapotajwa tena Machi 28 mwaka huu.