27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

WAFANYAKAZI MAJUMBANI WAMULIKWA

NA CLARA MATIMO

– MWANZA

LICHA ya sheria ya mtoto ya mwaka 2009 kuzuia watoto  wenye umri chini ya miaka 14 kuajiriwa majumbani, imeelezwa kuwa bado idadi kubwa ya watoto wenye umri huo wanaendelea kutumikishwa kwa kasi katika Jiji la Mwanza.

Hayo yamebainishwa katika utafiti uliofanywa hivi karibuni na  shirika lisilo la Serikali linalojihusisha na utetezi wa haki za mtoto anayefanya kazi za nyumbani na kupinga usafirishaji haramu wa mtoto la Wote Sawa lenye makao yake jijini Mwanza.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Angela Benedict, alisema  walifanya utafiti katika kata za Kitangiri, Kawekamo, Nyasaka na Kiseke zilizopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza na kubaini watoto wengi wanatumikishwa.

Angela alisema kuwa walifanikiwa kuwafikia wafanyakazi wa nyumbani wapatao 416 ambao kati ya hao, 14 walikuwa chini ya miaka 14 kinyume na sheria.

Alisema kati ya watoto hao 416, hakuna hata mmoja ambaye amesoma hadi kidato cha nne, 45 hawajafika elimu ya msingi, 171 hawakumaliza elimu ya msingi na 200 ndio wamemaliza elimu ya msingi.

Alisema baada ya kubaini bado kuna watoto wenye umri chini ya miaka 14 wanaajiriwa na kukosa masomo, shirika lake limeanzisha mradi ujulikanao kama ‘Paza sauti ya mtoto mfanyakazi wa nyumbani’.

“Lengo la mradi huu wa mwaka mmoja ambao unafadhiliwa na Shirika la Voice kupitia msaada wa Serikali ya Uholanzi, ni  kupinga ukatili na aina zote za unyanyasaji kwa mtoto anayefanya kazi za nyumbani ili kuhakikisha anapata stahiki zake.

“Anatakiwa kushirikishwa katika mambo mbalimbali ya kijamii, lakini tutautekeleza katika kata nne tu ambazo tulizifanyia utafiti,” alisema Angela.

Alisema mradi huo hauwezi kufanikiwa bila kuwashirikisha wadau mbalimbali, hivyo wamewakutanisha wafanyakazi wa nyumbani, waajiri wao, madiwani, watendaji wa kata, wenyeviti wa mitaa, viongozi wa dini na maofisa ustawi wa jamii wa Manispaa ya Ilemela wapatao 50.

Mmoja wa wafanyakazi wa nyumbani, Agnes Mkama,  alilishukuru Shirika la Wote Sawa kwa kumpa semina hiyo ambayo imemsaidia kutambua haki zake anazostahili kupewa na mwajiri wake, ambazo alikuwa hazijui ikiwamo kupewa likizo na mkataba.

Naye Diwani wa Kata ya Kawekamo, Japhesi Rwehumbiza (CCM), aliwataka waajiri kuhakikisha wanaajiri wafanyakazi walio na umri unaoruhusiwa kisheria kufanya kazi, huku akibainisha kwamba   kuanzia sasa viongozi wote  katika kata hizo ambao wamejengewa uwezo, watakuwa na ajenda moja ya kumlinda mfanyakazi wa nyumbani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles