23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

NEC YATUPA RUFAA YA UBUNGE SINGIDA KASKAZINI

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetupa rufaa iliyowasilishwa na mgombea ubunge wa Singida Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha AFP, Omari Sombi, akipinga uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo dhidi ya pingamizi alilomwekea mgombea wa CCM, Monko Joseph.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa NEC, Ramadhan Kailima, ilieleza kuwa kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 40(6) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 ikisomwa pamoja na kanuni za 34 na 35 za Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015, NEC ilipokea rufaa moja kutoka kwa mgombea wa ubunge Jimbo la Singida Kaskazini.

Mbali na hilo, pia NEC ilipokea rufaa mbili. Ya kwanza iliwasilishwa na mgombea wa udiwani Kata ya Keza – Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kwa tiketi ya CCM, Bakundukize Gwaibondo, akipinga uamuzi wa msimamizi  wa uchaguzi ngazi ya jimbo dhidi ya pingamizi alilomwekea mgombea wa NCCR – Mageuzi, Eradius Bitemele.

Na rufaa ya pili ilitoka kwa mgombea wa udiwani Kata ya Kwagunda – Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kwa tiketi ya CCM, Said Shenkawa, akipinga uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo dhidi ya pingamizi alilomwekea mgombea wa CUF, Yusuf Senkawawa.

Katika kikao chake cha kawaida kilichofanyika Desemba 24, mwaka huu, NEC ilipitia rufaa hizo na kufanya uamuzi.

“Kuhusu rufaa ya mgombea ubunge, tume imekubaliana na maamuzi ya msimamizi wa uchaguzi na hivyo mgombea aliyekatiwa rufaa aendelee kuwa mgombea wa ubunge Jimbo la Singida Kaskazini.

“Kuhusu rufaa za wagombea udiwani Kata ya Keza na  Kwagunda, tume imekubaliana na maamuzi ya wasimamizi wa uchaguzi na hivyo wagombea udiwani waliokatiwa rufaa waendelee kuwa wagombea wa udiwani katika kata husika,” alisema Kailima katika taarifa yake.

Alisema taarifa rasmi za uamuzi wa tume zimetumwa kwa wasimamizi wa uchaguzi ili wawapatie wahusika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles