24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

AJALI ZINAWEZA KUPUNGUA KWA MADEREVA KUFUATA SHERIA

MARA nyingi katika kipindi kama hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka matukio mengi ya ajali za barabarani yamekuwa yakiripotiwa.

Matukio hayo huwasababishia wananchi wengi madhara makubwa, ikiwamo vifo, majeraha makubwa na wengine hupata ulemavu wa kudumu.

Ajali hizo zimekuwa zikisababishwa na madereva wanaovunja sheria za usalama barabarani, ikiwamo kwenda kasi na wengine kuendesha magari mabovu.

Katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka ni vema madereva wakaongeza umakini barabarani, kwani idadi ya watu wanaosafiri kwenda mikoani ni kubwa.

Hata hivyo baadhi ya madereva wamekuwa na tabia ya kuendekeza starehe katika kipindi hiki, ikiwa ni pamoja na ulevi ambao huwafanya kupoteza umakini wawapo barabarani na hatimaye kusababisha ajali.

Wamiliki wa mabasi wenye tamaa ya fedha, nao wamekuwa wakitumia kuwapo wingi wa watu wanaotaka kusafiri, kuingiza barabarani hata mabasi yao mabovu jambo linalotajwa kuwa chanzo cha ongezeko la ajali katika kipindi hiki.

Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2017/18 Mei mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alisema katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 jumla ya matukio 6,500 ya usalama barabarani yaliripotiwa nchini.

Katika matukio hayo, alisema jumla ya ajali 1,552 zilisababisha vifo vya watu 2,372 na watu 6,074 kujeruhiwa.

Takwimu zinaonesha kupungua kwa ajali hizo kwa asilimia 7 kwani katika kipindi kama hicho mwaka 2015/16 kulikuwa na jumla ya ajali za barabarani 7,006 zilizoripotiwa ambapo watu 2,589 walipoteza maisha na 7,536 walijeruhiwa.

Alisema kwa ujumla ajali nyingi kati ya hizo zimesababishwa na uzembe wa madereva, kutozingatia sheria za usalama barabarani, mwendo kasi, ulevi pamoja na ubovu wa magari na miundombinu.

Katika mikakati ya kuzidi kupunguza idadi ya ajali nchini, wiki hii mabasi 20 kati ya 400 yaliyokuwa yakisafirisha abiria kwenda mikoani, yalizuiwa na askari wa usalama barabarani Kituo cha Mabasi Ubungo (UBT) kuendelea na safari, huku manne kati ya hayo yakisitishwa kutoa huduma ya usafiri kutokana na ubovu.

Mabasi hayo yaliyokosa sifa ya kusafirisha abiria, yalibainika baada ya askari wa kikosi cha usalama barabarani kituoni hapo kufanya ukaguzi.

Sisi wa MTANZANIA tunaamini kuwa ajali za barabarani za mara kwa mara zinaweza kupungua kwa madereva kufuata sheria za usalama barabarani na wakati huo huo askari nao watimize wajibu wao.

Tunasema hivyo kwa sababu baadhi ya askari wamekuwa chanzo cha matukio hayo pale wanapojihusisha na vitendo vya rushwa na kushindwa kuwachukuliwa hatua madereva wanaovunja sheria.

Kutokana na historia ya ajali nyingi kutokea katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, tunakishauri kikosi cha usalama barabarani kuongeza idadi ya askari wake katika barabara kuu.

Pia vituo vya ukaguzi wa magari barabarani viimarishwe  sambamba kutoa elimu ya usalama barabarani kwa njia za redio na luninga ili kuijengea jamii uelewa kuhusu namna bora ya kuzingatia kanuni na sheria za usalama barabarani.

Tunaamini hatua hizi zitasaidia kukabiliana na madereva wazembe wasiotaka kufuata sheria za usalama barabarani na kuendesha kwa umakini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles