28.4 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyabiashara Zingiziwa marufuku kando ya barabara

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, amewataka wafanyabiashara katika eneo la Zingiziwa kwenda kwenye soko lililotengwa kwani lina nafasi ya kutosha.

Akizungumza na wafanyabiashara hao baada ya kufanya ziara katika Soko la Zingiziwa ameagiza kukamatwa kwa wafanyabiashara wote wanaofanya shughuli zao kando ya barabara kwani tayari walishapewa maeneo rasmi.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Ubaya Chuma, akizungumza wakati wa mkutano wa wafanyabiashara wa Soko la Zingiziwa uliofanyika sokoni hapo.

“Nchi hii inaongozwa kwa taratibu za kisheria na zoezi la kuwapanga na kuelekezana wapi kila mtu akafanye biashara tulishalifanya, kwahiyo kitakachofuata kama mnarudi barabarani tutawakamata…nataka usawa kwa wananchi wote,” amesema Ludigija.

Aidha amesema wataendelea kuliboresha soko hilo pamoja na kufanya ukarabati wa barabara ili daladala ziweze kuingia muda wote biashara zifanyike vizuri.

Mkuu huyo wa wilaya pia amewataadharisha wavamizi wa maeneo ya watu na kuwataka wananchi kuwafichua ili kukomesha migogoro ya ardhi.

“Hatutaki migogoro ya ardhi ambayo inasababishwa na watu kwa makusudi, unaenda kwenye eneo ambalo unajua si la kwako unatengeneza muhuri feki, mwenyekiti feki, mnatengeneza barua za nyuma za kuonyesha kwamba eneo lilikuwa la nani ili kumtapeli mwananchi ambaye anamiliki kihalali. Hao wote nitapambana nao, nia yangu ni kukomesha matapeli wote wa ardhi,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Ubaya Chuma, amesema lengo la Serikali kuwapanga wafanyabiashara ni kutaka kurahisisha utoaji huduma za kijamii na kuwataka warudi katika maeneo yao.

Awali Diwani wa Kata ya Zingiziwa, Maige Maganga, amesema tayari wamepokea Sh milioni 100 kati ya Sh milioni 200 zilizotengwa kwa ajili ya uboreshaji wa soko hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles