Na Mwandishi Wetu -DAR ES SALAAM
WAFANYABIASHARA wadogo wa Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam wamemlilia Rais John Magufuli wakimtaka aingilie tozo mpya zinazotozwa kwao na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kwani zinaelekea kuwafilisi.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, wafanyabiashara hao wamedai kwa takribani wiki moja sasa wameshindwa kutoa hata kontena moja bandarini kwa sababu ya gharama kubwa wanazotozwa.
TBS imeanzisha utaratibu mpya wa kulipisha faini mizigo inayoingia hapa nchini ambayo haikukaguliwa wakati iko China, faini ambayo ni asilimia 15 ya thamani ya mzigo ulioingia.
Kwa kawaida, wafanyabiashara wadogo wa Kariakoo wana mitaji midogomidogo na hivyo huagiza mizigo kutoka nje kwa kushirikiana.
Lakini, kwa mujibu wa taratibu za TBS katika ukaguzi nje ya nchi, mizigo midogo yenye thamani ya chini ya dola 10,000 huwa haikaguliwia lakini inapofika Tanzania na kuonekana haijakaguliwa, wafanyabiashara hao hutozwa faini.
“Wafanyabiashara wengi wa Kariakoo ni wadogo. Hivyo hununua mizigo kidogokidogo na kuunganisha kupata shehena moja kubwa ili kuweza kupata nafuu ya gharama za kusafirisha. Hii imewezesha vijana wengi wenye mitaji midogo kushiriki kwenye biashara na kukuza mitaji yao.
“Kuna hatari ya sisi akinamama na vijana kukosa uwezo wa kuendelea kufanya biashara kutokana na hali hii. Tunatozwa tozo ya TBS asilimia 15 ya thamani ya mzigo (CIF ), kiwango ambacho ni chini kidogo ya VAT.
“Kwa hiyo kijana mwenye mzigo wa nguo zenye thamani dola 10,000 atalipa ushuru wa forodha asilimia 25, VAT asilimia 18, ushuru wa bidhaa asilimia 10 na TBS asilimia 15.
“Hii maana yake ni kwamba atalipa asilimia 68 ya thamani ya mzigo wake kama kodi ambayo ni sawa na dola 6800. Sasa kijana huyu atauza mzigo wake kwa shilingi ngapi?,” alilalamika mfanyabiashara Mohammed Mmasi wa Kampuni ya Mmasi Traders.
Akizungumza katika mkutano huo, mfanyabiashara mwengine, Sandaland Yenga, alisema wanamwomba Rais John Magufuli aingilie kati suala hilo kwani kama mfumo huo utaendelea, wafanyabiashara wadogo watafilisika.
“Utaratibu wa zamani wa wafanyabiashara wadogo kushirikiana uliwezesha vijana wengi wenye mitaji midogo kushiriki kwenye biashara na kukuza mitaji yao.
“Kuna hatari ya vijana hawa kukosa uwezo tena wa kuendelea kufanya biashara kufuatia Shirika la Viwango Tanzania kuwatoza Fedha nyingi sana za Ukaguzi wa ubora wa mizigo yao,” alisema.
Kwa sasa, biashara kubwa inayofanyika Kariakoo ni ile ya Watanzania kuagiza bidhaa kutoka China na kuziweka kwenye maduka yao na vifungashio vyao na halafu watu wa nchi jirani wanazinunua na kuzipeleka kwao. Nchi huingiza fedha za kigeni kwa njia hiyo.
Tanzania hivi sasa inafanya ukaguzi wa bidhaa zote zinazoingia nchini ili kudhibiti ubora ( pre shipment inspections). Ukaguzi huu unafanyika huko huko bidhaa zinaponunuliwa kabla ya kuletwa nchini.
Mwanzoni, bidhaa kama magari tu ndizo zilizokuwa zinakaguliwa lakini baadaye serikali ikaona ni bora kukagua bidhaa zote.
Kwa utaratibu huo mpya, hivi sasa shehena moja ya futi 40 inagharimu dola 260 kufanyiwa ukaguzi kwa wastani na inaweza kuwa juu zaidi ya hapo kutokana na thamani ya mzigo kwani tozo ya ukaguzi ni asilimia ya mali ( FOB ).
Wafanyabiashara hao walidai kwamba kwa muda wa wiki moja sasa, vijana na kinamama wa Kariakoo wanashindwa kutoa mizigo yao bandarini kwa sababu gharama imekuwa kubwa mno kwao.