25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

WAFANYABIASHARA MAILIMOJA WASINYANYASWE

NA GUSTAPHU HAULE -PWANI

DUNIANI kote hakuna nchi inayoweza kuendelea kiuchumi bila wafanyabiashara kuwekewa mazingira bora ya kufanya shughuli zao kwa uhuru bila kubughudhiwa.

Kama hivi ndivyo, leo hii nitagusia kidogo madhila wanayoyapata wafanyabiashara ndogondogo za matunda, samaki, chipsi katika eneo la Stendi ya Mailimoja katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani.

Ni takribani siku kadhaa sasa wafanyabiashara hawa wadogo wamekuwa wakihaha kutafuta maeneo ya kufanyia biashara zao nyakati za usiku kutokana na lile eneo walilokuwa wakifanyia mwanzo kufukuzwa na Halmashauri hiyo.

Ikumbukwe kwamba Stendi ya Mailimoja ni muhimu na maalumu kutokana na kuchangamka wakati wa usiku kwa sababu ni njia iendayo katika mikoa karibu yote ya Tanzania bara.

Kutokana na hilo, eneo hilo ni fursa adhimu kwa wakazi wa eneo hilo kubuni biashara ambayo wanaamini inatoka wakati wa usiku.

Wakazi hao ambao wengi ni masikini, wamekuwa wakibangaiza kwa kuendesha maisha yao kwa kuuza matunda ya kila aina, chakula, chips, maji na vinywaji baridi kwa wateja wanaopita katika eneo hilo usiku hususan madereva na wasafiri wanaopita katika eneo hilo usiku.

Wapo ambao wanasomesha watoto na wengine wameweza kujenga hata nyumba na kuwa na familia kupitia biashara hiyo kuanzia saa 12 jioni hadi saa 5 na wengine saa 7 na kisha hurudi makwao kupumzika.

Sasa hivi wamefukuzwa katika eneo hilo na kupigwa marufuku kufanya biashara yoyote wakati wa usiku, sasa maswali ya kujiuliza ni haya, je, kuna madhara gani yanayoletwa na wafanyabiashara hao au wanaathiri nini katika eneo hilo?

Niwakumbushe wataalamu wa halmashauri hiyo kwamba katika miji iliyoendelea, watu wanafanya kazi usiku na mchana. Suala la watu kufanya kazi mchana na kwenda kupumzika au kulala usiku linafanywa na mataifa yasiyojua maana ya uchumi ni nini.

Ndiyo maana hata wale waliopiga marufuku baa kufunguliwa asubuhi hawakufikiria nje ya boksi la uchumi. Si watu wote wanafanya kazi mchana.

Kuna watu usiku kucha wanatembea na magari, hao wakifika miji kama Mailimoja watapaki magari na kutafuta chakula au kinywaji, huku mfanyabiashara akifaidika na uchumi wa mtu mmoja mmoja na mwisho taifa zima kufaidika.

Hapa nakumbuka usemi usemao ‘aliyeshiba kamwe hawezi kumthamini mwenye njaa’, methali hii imeonekana wazi kutumiwa na viongozi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha. Ni jambo la hekima kujali na kuweka ubinadamu mbele kuliko inavyofanyika sasa.

Hivi kuwafukuza watu ambao wanajitafutia kipato na kupanda majani ambayo hayaliwi na binadamu na kuwaacha watu wakitaabika huku mkiendelea kukusanya ushuru kipi bora?

Viongozi mnapaswa kujitafakari upya ni kweli mnawataka kuhamia katika soko jipya la Loliondo, lakini je, huko mnakotaka kuwapeleka miundombinu yake ni rafiki kwa wao kufanya biashara wakati wa usiku?

Nani atakwenda usiku Loliondo kununua wali kwa mama na baba lishe au matunda?

Mnajua fika kutoka Mailimoja mpaka Loliondo usiku gharama yake kwenda na kurudi ni Sh 800 kwa dalala na bodaboda ni Sh 2,000.

Nani anaweza kutumia gharama hizo kufuata bidhaa ya Sh 500?

Mfanyabiashara ndogondogo anachukuliwa bidhaa zake kwa nguvu, anavunjiwa meza yake huku mtaji wake ukiwa ni Sh 50,000 au 100,000 tena akitakiwa kurejesha mkopo huo kila wiki.

Jambo hili halihitaji kiongozi mwenye cheti halisi ama cha kughushi, ni busara tu na kuangalia mantiki ya zuio hilo kwa wamachinga hawa.

Tusisubiri wanyonge hawa wakainua mabango kumweleza rais madhila wanayoyapata kutoka kwa viongozi waliopewa dhamana ya kuwasimamia.

Rais Magufuli amekuwa kiongozi wa pekee nchini kuwatetea wafanyabiashara hawa masikini ambao wanatafuta riziki kwa tabu na mara nyingi amekuwa akisema wasinyanyaswe, lakini mbona nyinyi viongozi Kibaha mnakiuka maagizo yake?

Mnataka rais wetu arudie tena kauli yake kwamba wafanyabiashara wasibughudhiwe? Au Kibaha haihusiki na tamko la rais?

Halmashauri ya Kibaha wapeni hawa watu utaratibu maalumu wa kufanya biashara katika eneo hilo, huku wakizingatia usafi pamoja na kulipa ushuru stahiki pale inapolazimika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles