27 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

WACHIMBAJI WANATAMANI ‘MADINI DAY’

CLARA MATIMO  – Mwanza

MWANZONI mwa mwezi huu,  Shirikisho  la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (Femata) kupitia Mkutano wake Mkuu wa tatu wa mwaka, ulitoa mapendekezo mbalimbali yatakayosaidia kutatua changamoto katika sekta hiyo muhimu.

Mkutano huo wa siku mbili  uliowakutanisha wadau mbalimbali  wa madini na watendaji wa Serikali uliobebwa na kaulimbiu ya Tanzania ya viwanda inawezekana kupitia uchimbaji wa madini.

Mkutano huo pia ulilenga kupokea na kujadili taarifa za maendeleo, mafanikio, changamoto na utekelezaji wa sera na sheria zinazoongoza sekta ndogo ya madini.

Binafsi nilifurahishwa na taarifa ya Rais wa Femata, John Bina, kwamba nchi yetu inayo madini zaidi ya 240, hata hivyo licha ya utajiri huo wote bado tunashuhudia changamoto na unyonge wa sekta hii katika kuinua uchumi wa Taifa letu.

Wakati hali ikiwa hivyo nchini mwetu, nchi kama Japan, Singapore na Ubelgiji  zisizotegemea rasilimali za madini kama tulizonazo sisi, zimewekeza na kuinua uchumi wao, swali la kujiuliza hapa ni je, sekta yetu ina matatizo gani.

Femata katika mkutano wao huo wanajaribu kutoa mapendekezo mojawapo ikiwa ni kuiomba Serikali kutenga siku maalumu ya madini ili kutoa nafasi kwa wadau wa sekta hiyo kukutana na kujadili changamoto zake, mafanikio na namna ya kuifanya sekta hiyo iwe mbele katika kuchangia pato la Taifa.

Binafsi, naliona pendekezo hilo ni jema na limekuja kwa muda mwafaka kwa sababu tumeshuhudia mambo mbalimbali yenye changamoto yakitengewa siku maalumu kwa ajili ya kumbukumbu, lakini kikubwa ni kwa wadau kupata nafasi ya kujadili kwa kina masuala yao.

Mathalani maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) yakitengewa maarufu kama siku ya ukimwi duniani, siku ya watoto, wanawake na mengine mengi.

Hivyo basi, sekta ya madini inayokadiriwa kuwa na wachimbaji wapatao milioni 4 hadi 6 mpaka nchini kote ambao wamekuwa wakiunga mkono kwa nguvu zote dhamira ya Rais Dk. John Magufuli ya kutetea rasilimali, wanakosaje fursa na siku yao ya kuzichambua changamoto, kupendekeza mwafaka wao namna gani sekta hii inabidi iendeshwe kwa kuliletea tija Taifa letu?

Wazo hilo la Femata linaleta faraja na kufufua matumaini kwa maana  kama tuna aina nyingi za madini kiasi hicho, kwanini tusiwe na siku maalumu ambayo itawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo?

Naamini Serikali yetu ni sikivu na italifanyia kazi ombi hilo kutoka kwa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania, ili kutoa nafasi kwa wadau wa sekta ya madini kujumuika pamoja angalau mara moja kwa mwaka na kujadili matatizo na mafanikio yao sambamba na kuyatafutia ufumbuzi kwa nia ya kusonga mbele na kujenga uchumi kupitia sekta ya madini ili kutekeleza sera ya Tanzania ya viwanda kikamilifu.

Nafurahi kwa jinsi ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano ilivyowapigania wachimbaji wadogo katika maeneo ya Kanda ya Ziwa Viktoria na kuwapa maeneo yao ambayo sasa hayaingiliwi tofauti na awali ambapo walinyang’anywa na wachimbaji wakubwa.

Naamini Rais Dk. Magufuli alitambua kwamba  hakuna nchi yoyote duniani ambayo itafanikiwa kupitia madini, ikiwa wazawa hawachimbi ndiyo maana akashikamana nao ili kuhakikisha wanajikwamua wenyewe na wanainua  uchumi wa nchi kwa sababu alijua Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe.

Nia hiyo ya dhati ya rais wetu imewatia hamasa wachimbaji wadogo kwa sababu hivi karibuni nimeshuhudia Mgodi wa dhahabu wa  Kapumpa uliopo Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, unaomilikiwa na wachimbaji wadogo ukiwa kinara kwa kulipa mrabaha (royalty) kwa miezi miwili mfululizo zaidi ya Sh milioni 30 kati ya migodi 617 iliyopo kanda ya kati Magharibi.

Hii inadhihirisha jinsi ambavyo wazawa wana nia ya kuinua uchumi wa nchi yao, hivyo kuwepo kwa siku hiyo maalumu ambayo tunaweza kuibatiza ‘Madini Day’, kutatoa fursa kwa wadau wote katika sekta hiyo kutoka sehemu mbalimbali nchini kukutana na kubadilishana mawazo na uzoefu wa utendaji kazi kuhusu uchimbaji madini kisha tutaweza kupiga hatua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles