NA FERDNANDA MBAMILA- DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Biashara na Viwanda, Charles Mwijage, anatarajia kufungua semina itakayowashirikisha wafanyabiashara 200 wa sekta ya ujenzi kutoka China.
Semina hiyo ya siku moja inatarajiwa kufanyika Novemba 25 mwaka huu na kuhudhuriwa na Balozi wa China nchini.
Habari zinasema mada zitakazo zungumziwa ni pamoja na mabadiliko ya bajeti ya mwaka 2016-2017.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, ilisema semina hiyo itawawezesha wafanyabiashara wa China kuzingatia na kuzitumia sheria juu ya kutoa kodi sahihi.
Alisema pia itawasaidia kukokotoa kodi ya uzio katika bidhaa na huduma na hivyo kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari miongoni mwao.
“Katika semina hiyo mada maalumu zitakazozungumziwa ni pamoja na mabadiliko ya bajeti ya mwaka 2016-2017, masuala ya forodha na uondoshaji wa bidhaa, kodi ya zuio katika sekta ya ujenzi na kodi ya ajira,” alisema Kayombo.
Wafanyabiashara hao watapata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu mambo mbalimbali kuwawezesha kufanya shughuli zao vizuri kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Pamoja na kuwasaidia katika masuala ya kodi semina hiyo inatarajia kuboresha uhusiano mzuri kati ya Tanzania na China.