24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyabiasha Kijiji cha Nkome wafurahia elimu ya Kodi mlango kwa mlango

Na Mwandishi Wetu, Geita

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imebaini changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wananchi wa Kijiji cha Nkome na vitongoji vyake mkoani Geita hasa ile ya kulazimika kusafiri umbali wa kilometa 60 kufuata huduma katika ofisi za TRA zilizopo Geita mjini.

Hayo yalizungumzwa na Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi kutoka makao makuu ya TRA, Rose Mahendeka katika kampeni ya Elimu ya Kodi mlango kwa mlango inayoendelea mkoani Geita.

Afisa Msimamizi Kodi Mkuu wa TRA, Rose Mahendeka, akimuelimisha mlipakodi wa eneo la Nkome mkoani Geita John Peter wakati wa Kampeni ya elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango mkoani hapo.

Alisema sambamba na kusfiri umbali mrefu, pia wamebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanafanya biashara wakiwa kwenye fremu lakini hawajasajiliwa na TRA na kwamba wameshawapa elimu.

Alisema katika kampeni hiyo wanatoa elimu ya Kodi, ulipaji Kodi, utunzaji kumbukumbu, matumizi ya mashine za kodi za Kielektroniki za EFD, pamoja na utoaji wa risiti kila baada ya kutoa huduma kwa mteja.

“Tupo mkoani Geita na tumeanzia vijijini katika kijiji cha Nkome na vitongoji vyake lakini lengo tuwafikie wananchi wote katika mkoa mzima ili tuwape elimu hii muhimu ya kodi.

“Kuhusu changamoto ya umbali pindi wanapofata huduma TRA, tumeichukua na tutaifanyia kazi ili kuwarahisishia kulipa na kukusanya kodi kwa urahisi lakini pia kuwawezesha kupata huduma zote za TRA kwa urahisi,” Rose.

Alisema wafanyabiashara wawapokee maafisa wa TRA kwani watanufaika na kampeni hiyo kwani pia watawaelimisha kuhusu haki zao pamoja na wajibu wao katika masuala yanayohusu kodi.

“Mfanyabiashara na Afisa wa TRA ni kama mgonjwa na daktari kwani ukificha hutoweza kupata elimu ya kiwango gani cha kodi unachotakiwa kulipa kwa usahihi,” alisema Rose.

Yusuph Bangayuka ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Nkome, alisema kuwa kampeni hiyo ina umuhimu mkubwa kwa wafanyabiashara kwani itawasaidia kujua namna ya kuendesha biashara zao.
Alisema wafanyabiashara wengi walikuwa wanaendesha biashara zao bila kuwa na uelewa kuhusu masuala ya kodi kutokana na kuwa hawajawahi kupata hiyo elimu hivyo zoezi hilo linatakiwa kuwa endelevu ili kuwawezesha kupata elimu bora na kuwajengea utayali wa kulipa kodi wa hiyari.

Naye John Peter ambaye ni mfanyabiashara katika kijiji cha Nkome, alisema kuwa amejifunza umuhimu wa kuwa na leseni, TIN pamoja na kutunza kumbukumbuku kila anapofanya mauzo ili kuchangia pato la serikali.

Alisema nchi bila mapato haiwezi kupata maendeleo hivyo kampeni hiyo ni muhimu kwani itakuwa ikiwakumbusha umuhimu wa kodi na kwamba hakuna nchi inayoendeshwa bila wananchi wake kulipa kodi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles