Na Mwandishi Wetu, Arusha
Wadau mbalimbali wanakutana jijini Arusha kwa siku sita kwa lengo la kuandaa mitaala miwili ya uanagenzi (apprenticeship), itakayotumika katika Chuo cha Maji.
Aidha, wadau hao wanaongozwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kushirikiana na Chuo hicho huku wadau wengine wakiwa ni Mamlaka za Maji za kitaifa ikiwemo RUWASA, NACTE, TCU na wasimamizi wa masuala ya usambazaji wa maji.
Akizindua kongamano hilo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Antony Sanga, amesema chuo hicho kimeona ni muhimu kufanya maboresho ambayo yatasaidia kuongeza ujuzi kwa wanafunzi na kuwaongezea uelewa zaidi.
Amesema lengo la mitaala hiyo mipya ni kuongeza zaidi elimu ya nadharia na vitendo hivyo kupitia wadau hao watajadili na kuona namna nzuri ya kuongeza mafunzo ya vitendo ili kuwasaidia kupata ujuzi zaidi na weza kushindana katika soko la ajira.
“Katika mageuzi ambayo tunaendelea nayo katika sekta hii muhimu ya maji,kuandaliwa kwa mitaala hii ni sehemu ya kufanya maboresho hayo ambayo itatusaidia kuboresha huduma ya maji kwa wananchi,”amesema Mhandisi Sanga.
Kwa upande wake Meneja miradi ya uendelezaji ujuzi kutoka ILO hapa nchini, Comoro Mwenda, amesema wamekuwa wakishirikiana na wadau mbalimbali nchini ikiwemo serikali ili kusaidia katika uendelezaji na upatikanaji wa ujuzi unaostahili hasa kwa vijana.
Amesema awali katika mradi huo wa kuongeza ujuzi,wanasaidia mafunzo ya uanagenzi kwa kushirikiana na serikali na taasisi husika za mafunzo ambapo walianza na Chuo cha Utalii tawi la Arusha na Dar es Salaam mwaka 2014.
Amesema Chuo hicho cha maji kilionyesha uhitaji wa msaada wa kitaalamu katika kuelewa masuala ya uanagenzi kutoka ILO ili waone namna watatengeneza mitaala hiyo itakayosaidia vijana kupata ujuzi zaidi.
Ameongeza kuwa mpango huo umelenga kusaidia vijana kuongezewa ujuzi kwani vijana wengi wamekuwa wakikutana na tatizo la ajira ambalo linakabili nchi nyingi barani Afrika.
Naye Mkuu wa hicho, Dk. Adam Karia amesema wamefanya tafiti mbalimbali kuangalia sababu zinazofanya vijana wengi kukosa ajira ambapo walibaini ni pamoja na wengi kutokuwa na maarifa ya kutosha wakiwa kazini hivyo kushindwa kuajiriwa au kujiajiri.
Alitaja mitaala hiyo kiuwa ni shahada ya kwanza katika uhandisi wa usafi wa mazingira (Bachelor degree in sanitation engineering) na stashahada ya matengenezo (Diploma in maintenance engineering).
Mkuu wa (NACTE) Kanda ya Ziwa, Godfrey Mhangwa alisema wanaamini mitaala hiyo ya uanagenzi itasaidia sana wahitimu ambao watatoka katika chuo hicho na vyuo vingine vitakavyoandaa mitaala ya namna hii.