Na Mwandishi wetu –
Wadau wa utalii nchini wametakiwa kuanzisha mipango maalumu itakayotoa elimu kwa waandishi wa habari juu ya masuala ya utalii na uhifadhi.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Januari 20, jijini Arusha na Ofisa Utalii wa mkoa huo, Flora alipokuwa akizungumza katika kongamano la tatu la masuala ya utalii na uhifadhi kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini na wadau wa utalii kutoka mikoa hiyo.
Amesema programu hizo zitasaidia waandishi wa habari wasipotoshe kuhusu masuala hayo lengo likiwa ni kukuza sekta hiyo muhimu ambayo inachangia kiasi kikubwa cha fedha za kigeni katika pato la taifa.
“Elimu hiyo itasaidia kutangaza utalii na uhifadhi na ushirikiano katika kupiga vita vitendo vya ujangili,” amesema.
Kongamano hilo limeandaliwa Taasisi ya wanahabari ya Arusha Media, ambapo mada mbalimbali zimejadiliwa zikiwamo uandishi bora wa habari za utalii, umuhimu wa uhifadhi, uwindaji wa kitalii, changamoto za waongoza watalii, umuhimu wa kutunzwa mapori ya akiba na maeneo yaliyohifadhiwa na umuhimu wa kutangaza utalii.