Susan Uhinga, Tanga
Wadau wa habari nchini, wamekutana jijini Tanga kujadili na kutoa mapendekezo ya kuweka mfumo wa kitaifa wa usalama kwa waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao ya kikazi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Novemba 30, Katibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, amesema katika mkutano huo wanahabari na wadau wa habari watajadili kwa pamoja namna bora ya kufanikishwa kuundwa kwa mfumo huo ambao una lengo la usalama wa mwandishi wa habari anapokuwa kazini ili kuongeza ufanisi.
“Nchini kwetu tumechelewa kuweka mfumo huu kwani nchi za wenzetu kama majirani zetu Kenya tayari umekwishafanyika,” amebainisha Mukajanga.
Amesema mfumo huo utamsaidia na kumlinda mwandishi wa habari anapokuwa kazini kufanya kazi kwa ufanisi na katika mazingira salama.
Mambo mengine yanayojadiliwa ni pamoja na uhuru wa uhariri na sheria zinazokinzana.