Na MASYAGA MATINYI – SIMANJIRO
WACHIMBAJi wadogo wa tanzanite wamelalamika kukosa nafasi ya kumweleza Rais John Magufuli upande wao juu ya biashara ya madini hayo, huku wakipinga takwimu zilizotolewa na Kamati Maalumu ya Bunge iliyochunguza uendeshaji wa uchimbaji wa madini hayo.
Akizungumza mjini Mererani, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimba Madini Mkoa wa Manyara (Marema), Jafari Faraji, alisema waliandaa risala yao waliyotarajia kuisoma mbele ya Rais Magufuli, wakati alipofanya ziara katika mji mdogo wa Mererani, mkoani Manyara, Jumatano iliyopita na kuagiza kujengwa ukuta kuzunguka eneo hilo.
Kupitia risala hiyo (nakala tunayo), wanasema kati ya Julai, mwaka juzi hadi Februari, mwaka huu, walizalisha na kuuza asilimia 23 ya tanzanite yote ambapo kiasi kilichoripotiwa ni kilogramu 240 dhidi ya asilimia 77 iliyozalishwa na kampuni kubwa.
Kamati ya Bunge iliyoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, katika ripoti yake iliyotolewa Septemba 7, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dotto Biteko, alisema tangu mwaka 1998 ni kilogramu 13 tu za tanzanite ndizo zimerekodiwa.
“Biashara ya tanzanite imegubikwa na wizi mkubwa na takwimu zinaonyesha kuwa tangu mwaka 1998 ni kilo 13.2 tu za tanzanite zimezalishwa nchini, sawa na kuzalisha gramu 700 za tanzanite kwa mwaka kwa kipindi chote cha miaka 19,” alisema Biteko.
Alisema katika risala yao walikusudia kumweleza Magufuli changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo na mchango wao katika pato la taifa.
Kuhusu kodi, alisema miaka ya nyuma elimu ya kodi ilikuwa ndogo, lakini kwa sasa wapo tayari kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) au taasisi yoyote ile ya Serikali inayojihusisha na ukusanyaji wa mapato.
“Kutokana na uzalishaji huo, wachimbaji wadogo na wa kati kwa pamoja walilipa zaidi ya Sh milioni 224.2 zikiwa ni mrabaha uliotokana na mauzo ya madini yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 4.8.”
DC ajibu
Akizungumzia wachimbaji wadogo kutopata fursa ya kusoma risala mbele ya Magufuli, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula, alisema hawakunyimwa fursa, bali ratiba haikuruhusu.
“Kwa kweli ratiba ilibana, hata mimi DC sikupata fursa hata ya kusalimia wananchi, lakini bado wana nafasi ya kufikisha ujumbe wao kwa Rais kupitia sisi wasaidizi wake,” alisema.
Waomba muda zaidi
Wachimbaji hao wameomba kuongezewa muda ili kuweza kuwasilisha vielelezo vinavyotokana na waraka kutoka kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, waliokabidhiwa Septemba 15, huku ukiwa na maswali 34 waliyotakiwa kuyajibu yote ndani ya siku tatu.
Baadhi ya wachimbaji wamedai waraka huo una lengo la kuwafutia leseni na kuwaondoa kabisa katika biashara ya tanzanite.
Waraka huo unaotoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, unalenga kukusanya maelezo ya wachimbaji wa madini hayo.
Maelezo yanayotakiwa na dodoso hilo ni jina na mgodi/kampuni na namba ya leseni, ulianza uchimbaji mwaka gani, wakurugenzi wa kampuni, aina ya madini yanayochimbwa, madini kiasi gani yameripotiwa kutoka kuanza uchimbaji, idadi ya wafanyakazi na idadi ya waajiriwa wa kudumu.
Pia inataka mwenye kitalu aeleze idadi ya ajira za muda, kiasi wanacholipwa kwa siku, kiasi wanacholipwa kwa mwezi, mkataba wa mwajiriwa ukoje, wafanyakazi wangapi wanalipiwa katika mifuko ya jamii, aina ya mifuko ya jamii wanayolipiwa, utawala wa mgodi ukoje, ukubwa wa eneo linalochimbwa, ni kiasi gani kinachimbwa, uzalishaji ni kiasi gani kwa siku, mwezi na mwaka.
Wanatakiwa pia kueleza kodi inayolipwa serikalini, mrabaha asilimia 6 kiasi gani, service levy Wilaya ya Simanjiro ni kiasi gani, mazao yanayopatikana yanauzwa wapi, ni nani mnunuzi mkubwa na wanunuaji wengine na wapi lilipo soko.
Maswali mengine ni namna wananchi wa eneo husika wanavyofaidika na uchimbaji, kiasi cha kodi iliyolipwa Serikali Kuu, Serikali ya Wilaya ya Simanjiro na Serikali ya Kijiji au mji mdogo wa Mererani.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk. Joel Bendera, alikiri ofisi yake kutoa waraka huo, ambao ameuita dodoso.
Dk. Bendera alisema haoni sababu yoyote kwa wachimbaji kuwa na hofu juu ya waraka huo, kwa madai kwamba umeandaliwa kisayansi.
“Tunataka tuwafahamu ili tuwasaidie, kama mtu yupo sawa sawa katika shughuli zake, basi siku nne ni nyingi na zinatosha kabisa kuwasilisha vielelezo vyote, sasa wanaodai muda ni mfupi kwani dodoso hiyo ni mtihani?” alihoji.
Kuhusu dodoso hiyo kuhusishwa na vita ya kimaslahi kati ya wawekezaji kwenye machimbo ya tanzanite ambao ni Kampuni ya Sky Associates Group Limited, Dk. Bendera alisema hakuna kitu kama hicho, kwa sababu hata wao (wawekezaji) wanapaswa kujibu maswali yote.
Huku ni kushindwa kazi. Hivi kweli watu mpo serious na kazi, maisha na usalama wa nchi na watu. Mtu yuko na kiwewe unamwambia ndo mwenye jibu. Inamaana ukuvamia wewe ndo uwe mhusika mkuu wa uvamizi huo. Na hata ukipigwa. Sasa kazi ya kiinteligensia ni nini.Basi hatuhitaji polisi kama mambo ndo hivi. Tunapewa mujibu wa kujifanyia utafiti sisi wenyewa. Mmesikia shambulizi la marekani sijui kama mnafuatilia jinsi polisi walivyojua wapi yupo na akajifyatua mwenyewe. Huku ilitumika nusu saa, na sifahamu kama Polisi kwa mara moja walianza upelelezi au la. Watu na Wananchi si kuku jamani.