23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wachimbaji wadogo madini waandamana Simiyu

Na Derick Milton, Simiyu

Mgogoro wa mara kwa mara kati ya wachimbaji wadogo wa madini, watu wanaopewa leseni za uchimbaji na tume ya madini katika mgodi wa Bulambaka ulioko katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu umeingia katika sura mpya.

Mgogoro huo umewalazimu wachimbaji wadogo kuandamana katika Ofisi ya Mkuu wa wilaya na mkuu wa Mkoa, huku wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe wa kumkataa mwekezaji aliyepewa leseni ya uchimbaji kwenye mgodi huo.

Wakiongea na waandishi wa habari, wachimbaji hao wakiwemo wamiliki wa mashamba, wamesema wameamua kufanya maandamano ili kupaza sauti zao kwa viongozi wakuu wa taifa.

Wamesema kuwa hatua zilizotumika kupatikana kwa mwekezaji huyo, kumekuwa na usiri mkubwa, huku wakitaja uwepo wa viashiria vya rushwa katika upatakanaji wake.

“Kwanza hii leseni imetolewa haraka haraka katikati ya kipindi cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais John Pombe Magufuli, tulijiuliza kwa nini itoke sasa hivi na kwa haraka kiasi hicho,  pia tulipouliza wakasema huu ni utawala mpya siyo ule wa zamani wa Rais Magufuli,” amesema mchimbaji mdogo wa madini, Nyakelenge Gidioni.

Hata hivyo wachimbaji hao wamesema kuwa, wamiliki wa mashamba katika mgodi huo kwa muda wa mwaka mzima, wamekuwa wakiangaikia wapate leseni yao kutoka tume ya madini licha ya kukamilisha taratibu zote za uombaji.

“Tuliambiwa tuunde kikundi ili na sisi tupatiwe leseni ya uchimbaji, leo hii takribani mwaka mzima tumeangaika kupata hiyo leseni lakini tumeshindwa, mwekezaji aliyepewa leseni yeye ameomba hivi karibuni na amepata haraka haraka wakati sisi tumeangaika mwaka mzima,” amesema mchimbaji mdogo wa madini, Masuka Sahani.

Aidha wachimbaji hao wamesema mwekezaji huyo aliyepewa leseni, amekuwa na tuhuma za vitendo vya unyanyasaji, pamoja na wizi wa madini ambapo walieleza amewahi kukamatwa akitorosha mawe yenye madini.

Mkuu wa Wilaya, Festo Kiswaga aliongea na wachimbaji hao na kusema Ofisi yake haitambui leseni hiyo na wala hawezi kuongea jambo lolote juu ya mgogoro huo kwa sababu alitoa maelekezo na yameshindwa kutekelezeka na ofisi ya madini mkoa.

“ Mimi najua kila kitu kinachoendelea pia hiyo leseni imetoka kinyemela na ofisi yangu haitambui, ila siwezi kusema lolote, nendeni kwa mkuu wa mkoa, maana ofisi yangu imeshindwa kwani nimetoa maagizo ila wamegoma kutekeleza,” amesema mkuu wa wilaya, Kiswaga.

Pia mwekezaji huyo, Hussen Makubi aliapata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari juu ya tuhuma hizo na kusema kuwa yeye na wenzake wanaounda kikundi cha Buruwadu 4 Mine ndiyo wamepewa leseni ya kuchimba kwenye mgodi huo.

“Siyo kweli kuwa mimi ndiye nimepewa leseni, ila ni kikundi ambacho wapo na wenye mashamba, mimi ni mwenyekiti wa kikundi, tupo watu 39 na hizo tuhuma siyo kweli, tulifuata taratibu zote zinazotakiwa,” amesema Mwekezaji Makubi.

Makubi amesema kuwa leseni hiyo amepewa kihalali na hakuna vitendo vya rushwa kama wachimbaji hao walivyodai, huku akiiomba serikali kuingilia kati kwani shughuli za uchimbaji zimesimama kwa sasa.

Hata hivyo alipotafutwa Ofisa Madini hakuweza kupatikana kwa haraka, kwani alikuwa kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama mkoa kilichokuwa kikiendelea katika ofisi ya mkuu wa mkoa kujadili suala hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles