DIRISHA la usajili kwa timu za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na Daraja la Pili kwa msimu wa 2018/2019, linatarajiwa kufungwa Julai 26, mwaka huu kwa kutumia mfumo mpya wa usajili ujulikanao kama TFF FIFA Connect.
Dirisha hilo la usajili lilifunguliwa Juni 15, mwaka huu na tayari timu zinazoshiriki Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili zipo kwenye hekaheka za kufanya usajili kwa ajili ya msimu mpya.
Baada ya dirisha hilo la usajili kufungwa, kutakuwa na wiki moja ya pingamizi kuanzia Julai  27, mwaka huu ikifuatiwa na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kukaa kupitisha usajili huo.
Katika kipindi hiki cha usajili, mambo mengi hujitokeza na hata wakati mwingine wachezaji kujisajili kwenye timu zaidi ya moja na hivyo kusababisha mvutano baina ya timu hizo.
Ni jambo lililozoeleka kwa timu za Tanzania kusikia mchezaji mmoja kujisajili zaidi ya timu moja na hivyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kuamua hatima ya mchezaji aliyefanya jambo kama hilo na kufungiwa baada ya kupitia usajili wake na kujiridhisha.
Lakini wakati mwingine timu hufanya udanganyifu wa saini za mchezaji na jambo kama hili TFF hutoa maamuzi ya mchezaji kuchezea timu ambayo amefanya usajili halali.
Masuala ya usajili kwenye soka la Tanzania hasa mchezaji kujisajili zaidi ya timu moja, yamekuwa ni mambo ya kawaida na yanarudisha nyuma maendeleo ya mchezo huo wakati taratibu za usajili zipo wazi.
Mambo kama haya kwenye usajili yanasababisha migogoro baina ya timu moja na nyingine kuingia katika vita ya kuwania mchezaji.
Ni wakati wa wachezaji wenyewe kuepuka kuingia katika migogoro ya usajili katika kipindi hiki ambacho zimebaki siku chache kuelekea kufungwa kwa dirisha la usajili nchini.
Sisi MTANZANIA tunawaasa wachezaji kuwa makini na wajiepushe na kuingia kwenye migogoro isiyokuwa na lazima katika kipindi hiki cha usajili, kwani kitendo cha kushawishiwa na kujisajili zaidi ya timu moja kitawasababishia kufungiwa kucheza soka.
Si jambo jema hata kidogo kwa mchezaji kujisajili kwenye timu zaidi ya moja, kufanya hivyo ndio chanzo cha migogoro baina ya timu moja na nyingine, ni vema mchezaji kufanya maamuzi kabla ya kuamua timu anayotaka kuchezea kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Vitendo vya wachezaji kujisajili kwenye timu zaidi ya moja vimekuwa vikijirudia kila msimu na jambo kama hili linapaswa kukemewa na kupigwa vita ili lisijitokeze kwenye soka la Tanzania kwa ujumla.
Ipo haja ya TFF kuendesha semina kila baada ya msimu kwa wachezaji wanaocheza Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili ili kuwapa elimu kuhusiana na masuala ya usajili ili kuepuka udanganyifu na kujisajili kwenye timu zaidi ya moja.
XXXXX