30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wachezaji hawa watatisha tena msimu huu?

Mohamed Hussein ‘Tshabalala’
Mohamed Hussein ‘Tshabalala’

NA ZAINAB IDDY,

LIGI Kuu Tanzania Bara msimu wa 2016/17 unaoshirikisha timu 16, tayari umeanza kutimua vumbi tangu mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kwa sasa hivi mchezaji mmoja mmoja au timu kwa ujumla wapo katika vita ya kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi ya msimu uliopita.

Kwenye ligi iliyopita tuliona jinsi kulivyokuwa na upinzani wa mchezaji mmoja mmoja kiasi cha kuzua maswali mengi kwa wadau juu ya nani atatwaa tuzo mwishoni mwa msimu.

Miongoni mwa waliong’ara ni wachezaji wazawa ambao licha ya ushindani ulioonekana baina yao na wageni lakini waliweza kuonyesha kiwango bora, swali ni je, msimu huu watatisha tena?

Juma Mahadhi

Hakuna asiyejua uwezo wa Mahadhi akiwa uwanjani, licha ya muda mfupi alijiunga na Yanga na kuichezea mechi mbili za kimataifa za Kombe la Shirikisho.

Mahadhi amejiunga na Yanga akitokea Coastal Union ya mjini Tanga, baada ya kuonesha uwezo mzuri na kuwa mwiba kwa wapinzani licha ya timu hiyo kushuka daraja.

Ubora wake uwanjani ulipelekea kuzigonganisha timu za Simba na Yanga katika usajili, lakini mwisho akaangukia mikononi mwa Wanajangwani waliomfunga miaka miwili kwa dau la milioni 35.

Tayari amewateka mashabiki wa timu hiyo, kutokana na uwezo alioonyesha kwenye michezo miwili ya Yanga, akianza na ule wa TP Mazembe kabla ya Medeama, kwa sasa anaaminika kwenye kikosi cha Yanga lakini je, ataweza kung’ara kama ilivyokuwa Coastal Union msimu uliopita katika ligi hii?

Shiza Kichuya

Kiungo mpya mshambuliaji wa Simba, aliyejiunga na timu hiyo katika kipindi hiki cha usajili akitokea Mtibwa Sugar.

Msimu uliopita Kichuya aling’ara katika ligi na mashindano ya mapinduzi, jambo ambalo limemwezesha kupata tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Machi kwenye ligi ya msimu uliopita.

Mbali na kupata tuzo hiyo, kiwango chake kiliweza pia kumpa nafasi ya kuwa miongoni mwa wachezaji walioingia katika kinyang’anyiro cha uchezaji bora wa msimu na ule wa mchezaji bora chipukizi ambazo hakubahatika kupata.

Licha ya kutopata tuzo kutoka kwa wadhamini wa ligi, bado Simba wamemsajili ili kupata huduma yake, kikosi ambacho kinaushindani mkubwa na Yanga.

Mudhamir Yasini

Kiungo mpya wa Wekundu wa Msimbazi, amejiunga katika kikosi hicho hivi karibuni baada ya kuonesha kiwango bora katika ligi iliyopita.

Mudhamir amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Mtibwa Sugar, lakini akitarajiwa kukutana na changamoto kubwa ya namba hususani kutoka kwa Jonas Mkude.

Hassan Ramadhan

Beki huyo wa kulia wa Yanga anaupinzani mkali na Juma Abdul ambaye wanacheza namba moja.

Kessy amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Simba alikoitumikia kwa kipindi cha miezi 17 kati ya 18 aliyopewa.

Beki huyo ambaye ni zao la Mtibwa Sugar, alilazimika kuitumikia Simba kutomaliza mkataba wake wa kuitumikia timu hiyo baada ya kusimamishwa kwenye michezo mitano ya mwisho ya ligi kutokana na kumchezea vibaya Edward Christopher wa Toto iliyopelekea apewe kadi nyekundu.

Licha ya kuingia mgogoro na Simba ambao umesababisha kutoitumikia Yanga kwa muda, lakini uwezo wake haujifichi na ndicho kilichowashawishi Wanajangwani kumsajili, lakini swali ni kwamba ataweza kumweka benchi Abdul na kuyaendeleza makali yake?

Juma Abdul

Alistahili kupewa tuzo cha uchezaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, kutokana na juhudi zake alizozionyesha katika kuhakikisha timu yake ya Yanga inapata mafanikio.

Abdul ambaye amewabwaga Kichuya na Tshabalala katika tuzo hizo, ameiwezesha timu yake kutwaa ubingwa wa ligi, kombe la TFF lakini pia kutinga hatua ya makundi kwenye michuano ya kimataifa ya Shirikisho.

Katika ligi iliyopita, Abdul aliteuliwa pia kuwa mchezaji bora wa Aprili na kutwaa kitita cha Sh milioni moja baada ya kuwashinda Donald Ngoma kutoka Yanga na Hassan Dilunga wa JKT Ruvu.

Mohamed Hussein ‘Tshabalala’

Msimu wa 2015/16, ulikuwa wa mafanikio kwa beki huyo wa Simba baada ya kujinyakulia tuzo tatu tofauti zilizotokana na ligi.

Katika ligi iliyopita, Tshabalala alionekana kutokuwa na mpinzani wa kudumu ndani ya Simba na hivyo kuweza kuitumikia vilivyo hadi kuiwezesha kumaliza ikiwa kwenye nafasi ya tatu.

Kinda huyo aliyetengenezwa na Wekundu wa Msimbazi chini ya kocha Seleman Matola, alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi  Oktoba kwa timu yake, lakini pia amefanikiwa kutwaa ile ya msimu mzima baada ya kupigiwa kura na mashabiki wa Simba.

Kiwango kizuri cha Tshabalala kimemwezesha pia  kuingia kwenye kinyang’anyiro cha mchezaji bora wa msimu pamoja na mchezaji bora chipukizi ambacho amepata tuzo yake.

Bado mashabiki wa Simba wanamwamini kijana wao kuwa ana nafasi ya kuisaidia timu hiyo, lakini usajili uliofanywa kipindi hiki cha usajili unaweza kumweka katika wakati mgumu wa kuendelea kuwa kwenye ubora wake wa msimu uliopita.

Farid Mussa

Licha ya kutopata tuzo yoyote msimu uliopita, Farid ni moja ya wachezaji walioweza kuonyesha kiwango kizuri uwanjani msimu huo.

Farid aliingia katika kinyang’anyiro cha mchezaji bora chipukizi na wadau wengi walionekana kutupa karata kwake lakini hali ikawa kinyume baada ya kwenda kwa Tshabalala.

Kupewa tuzo hiyo Tshabalala kuliwafanya wanamichezo wengi hususani wa soka kupaza sauti zao wakidai kuwa hakustahiki, hii inaonyesha ni jinsi gani uwezo wa Farid uliweza kuonekana na wengi.

Licha ya changamoto hiyo, bado ana nafasi ya kujituma na kutwaa tuzo zaidi ya hiyo, licha ya kuonekana huenda atakata tamaa.

Mbali nawachezaji hao wapo pia Deogratius Munishi ‘Dida’  (Yanga), Miraji Adamu (alikuwa Coastal), Hassan Hatibu (Toto African msimu uliopita), Ibrahim Ajib (Simba), Aishi Manula na Shomari Kapombe (Azam FC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles