Na WAANDISHI WETU
WABUNGE wametakiwa kuondokana na hofu ya kifo na badala yake wamwombe Mungu, hasa wakati huu ambao kuna taarifa za matukio ya watu kutekwa na wengine kutishiwa maisha yao.
Kauli hiyo ilitolewa mjini Dodoma jana na Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk. Dickson Chilongani, alipoongoza Ibada ya Ijumaa Kuu ya kutafakari maneno ya Yesu msalabani iliyofanyika Kanisa Kuu la Anglikana.
Dk. Chilongani alisema kuwa, Mungu alikubali kumtoa mwanawe wa pekee ahukumiwe kwa ajili ya dhambi za walimwengu na hivyo hofu ya kifo na kutekwa haifai kuwapo na wote wenye hofu hiyo hawana Mungu mioyoni mwao.
“Kama wabunge wamekuwa na hofu ya kifo, je, sisi wengine tutakuwa na hali gani? Nawaomba wananchi wasikumbwe na hofu hiyo na wasiingie kwenye malumbano yasiyo na tija na badala yake wajikite kumwamini Mungu,” alisema.
Aliwatahadharisha Watanzania kuacha kuchanganya dini na siasa na kusema kufanya hivyo wanakiuka maagizo na mapenzi ya Mungu.
Pia aliwataka viongozi wa dini kutotumia muda wao mwingi katika siasa na kusema jukumu lao ni kuwa karibu na waumini wao na kuwatoa hofu na vitisho vilivyotawala.
“Jukumu lingine la sisi viongozi wa dini ni kuwaonea huruma na kuwaombea watu wanaowaudhi wengine kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kuyatii makusudi ya Yesu kufa msalabani,” alisema.
ARUSHA
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Solomon Masangwa, amewataka Watanzania wote kumuombea Rais Dk. John Magufuli na viongozi wote wa Serikali kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu.
Akizungumza mjini hapa jana, katika Ibada ya Ijumaa Kuu iliyoandaliwa na Umoja wa Makanisa Arusha na kufanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa hapa, alisema kila Mtanzania kwa imani yake akishiriki kuomba kwa ajili ya viongozi watasaidia kukuza ustawi wa Taifa letu.
“Rais wetu aliwahi kuweka ombi kwa Watanzania, tumuombee na sidhani kama kapotezea, kama hakupotezea basi tuendelee kumuomba Rais wetu na viongozi wote ili taarifa wanazozipokea wazitumie kwa ustawi wa nchi yetu na kuna usemi unaosema alivyo kiongozi ndivyo walivyo watu wake.
“Leo (jana) katika ibada hii tumeweka ombi la kuombeana, kuombea Serikali, kanisa na mkoa wetu, kwa hiyo viongozi wa dini na waumini wa dini zote tushirikiane katika hili,” alisema.
Akizungumzia kauli mbiu ya Serikali ya hapa kazi tu, alisema moja ya kazi hiyo ni kupeleka taarifa nzuri za maendeleo katika Taifa letu na kuwataka viongozi kuchuja baadhi wanazopelekewa na zisizo na maslahi kwa Taifa wasizifanyie kazi.
Alisema utoaji wa taarifa njema utasaidia viongozi kufanyia kazi taarifa nzuri na kudumisha amani katika nchi yetu.
“Mfano habari ya Rais ya kuzindua reli inayotoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ni taarifa njema na baada ya kusikia taarifa hiyo na sisi wa Kanda ya Kaskazini tunasema reli yetu ya huku nayo ianze kushughulikiwa ili iimarishe uchumi na mawasiliano katika nchi yetu.
“Lakini wapo wengine wanaochonganisha watu, wanasema hiyo ni kazi, wengine wanaiba na wanasema hiyo ni kazi, wanaua na kuwatesa watu wengine, wanapora nyara za Serikali wanasema ni kazi, hiyo si kauli mbiu ya taifa,” alisema.
Katika ibada hiyo kulifanyika maombi ya aina nne, ikiwamo kumuombea Magufuli na viongozi wote, kuomba kwa ajili ya mvua katika baadhi ya maeneo ambayo hainyeshi na maombi kwa ajili ya watoa taarifa kwa njia ya ishara, maandishi, mazungumzo na vyombo vya habari.
Awali, mgeni rasmi katika ibada hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema kukaa kwa pamoja kwa viongozi wa dini ya Kikristo kutoka madhehebu mbalimbali ni funzo kwa watendaji wa Serikali na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa la kushirikiana kwa pamoja bila kujali itikadi zao kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Kuhusu amani, alisema bila viongozi wa dini kuihubiri, Arusha na nchi nzima isingetawalika wala kukalika.
“Huu ni mkoa wa kitalii na mapato ya sekta hiyo zaidi ya asilimia 80 yanatokana na utalii wa hapa, hivyo Serikali tunajitahidi kuhakikisha tunadumisha amani iliyopo hapa nchini.
“Kuhusu maombi kwa Rais ni muhimu kwa sababu Rais anahitaji maombi wakati huu kuliko wakati wowote, kwa sababu ameamua kufanya mageuzi, hivyo tunahitaji kumtia moyo kwa sababu amesaidia mambo mengi, ikiwamo nidhamu kwa watumishi wa umma.”
KILIMANJARO
Naye Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Fredrick Shoo, amelitaka Taifa na Bara la Afrika kwa ujumla kutubu dhambi za ubinafsi, ukabila, ukanda na matumizi mabaya ya madaraka, jambo litakalosaidia kuondokana na laana kutoka kwa Mungu.
Akizungumza katika Ibada ya Ijumaa Kuu, alimpongeza Magufuli kwa hatua mbalimbali anazoendelea kuchukua katika kupamba na mafisadi wanaohujumu rasilimali za nchi.
“Nchi nyingi katika Bara letu la Afrika hazina uzalendo, tunaacha rasilimali zetu zinaporwa kama vile nchi hazina wenyewe, tena wanashirikiana na watu wanaowaita wawekezaji, jambo hili halifai,” alisema.
Alisema baadhi ya viongozi wa Afrika hawaheshimu matakwa ya sheria na wengi wao wakikataa kupokea ushauri wa watu na kuongoza kwa mabavu.
DAR ES SALAAM
Kwa upande wake, Askofu Mkuu Mstaafu wa KKKT, Dk. Alex Malasusa, amewataka watu wawe na utamaduni wa kusameheana ndani ya jamii kwa sababu kuwekeana chuki si vizuri kwa afya.
Kauli hiyo aliitoa katika Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika Kanisa la Azania Front na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, Edward Lowassa na mke wa Rais Mstaafu, Anna Mkapa.
Alisema watu wangesameheana, Taifa zima lingekuwa na furaha kwa sababu wana mioyo ya kusamehe.
“Hata Yesu alipokuwa msalabani alisema wasamehe hawa kwa sababu hawajui walitendalo, hata wale wanaotenda mabaya tuendelee kuwasamehe kwa sababu hawajui walitendalo,” alisema.
Malasusa alisema dhambi inakula watu hadi leo kutokana na kushindwa kufanya matendo mazuri yanayompendeza Mungu.
Alisema hawatakiwi kufanya jambo kwa kuwafurahisha watu, bali wanapaswa kufanya haki kwa kila mtu kama amekosea.
“Kwa mfano, Pilato alitumia hila za binadamu kwa kushindwa kutenda haki kwa Yesu, aliyekuwa hana hatia, alifanya hivyo kwa sababu ya kuwafurahisha watu, hivyo si mambo yote yanayoamriwa kwenye kura ndiyo,” alisema.
Pia alisema Watanzania wote wanatakiwa wapendane kwa sababu kwa Mungu hakuhitaji fedha, uongozi wa kanisa na madaraka yoyote, bali matendo yako ndiyo yatakupeleka kwa Mungu.
Aliwataka Wakristo kuendelea kumuomba Mungu kwa sababu Ijumaa Kuu haitoshi kwa kuvaa nguo nyeusi na si fasheni, bali ni siku ya historia kiroho.
Katika misa nyingine ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, waumini wa madhehebu ya Kikristo wametakiwa kutumia Sikukuu ya Pasaka kuunganisha jamii na si kuichonganisha na kuigombanisha.
Akizungumza katika misa hiyo, Padri Juvenalis Baitu alisema waumini na jamii kwa ujumla inapaswa kuepuka kusambaza ujumbe wa chuki, uongo na wenye lengo la kugombanisha watu.
Aliwataka waumini kuondokana na imani ya midomoni tu, bali iwe ya matendo itakayosaidia kudumisha upendo miongoni mwa familia na jamii kwa ujumla.
“Tusiwe watu wa kusambaza maneno ya chuki, uongo na yenye kugombanisha watu kwenye jamii. Tusambaze ujumbe wa kuunganisha na si kuchonganisha,” alisema.
Baitu alisema waumini wanapaswa kutumia uso wa Kristo kuleta upendo na amani baina ya mtu na mtu na jamii yote.
Naye Kasisi wa Kanisa la Mtakatifu Albanus Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jackson Sosthenes, amewaasa waumini wa Anglikana kuacha matendo ya kumchukiza Mungu na badala yake watende matendo mema kuishika Injili.
Alisema Pasaka inatoa mwanga kwa Wakristo kuona upendo wa Yesu na wanadamu wanapaswa kutenda mema siku zote.
“Kama Wakristo wa kweli na wenye imani, tujiulize juu ya ukombozi wa kazi ya Yesu Kristo alipokuja duniani kutukomboa dhidi ya dhambi zetu,” alisema Sosthenes.
Habari hii imeandikwa na Sarah Moses (Dodoma), Janeth Mushi (Arusha), Upendo Mosha (Kilimanjaro), Esther Mnyika, Ferdnanda Mbamila, Leonard Mang’oha na Harieth Mandari (Dar es Salaam)