31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

THBUB, CHADEMA, THRDC WAMTAKA IGP ATAFUTE KIINI

Na WAANDISHI WETU-DAR

VYAMA vya siasa pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya haki za binadamu nchini, wamemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kutafuta kiini cha mauaji ya askari polisi ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema shambulio dhidi ya askari wanane lililotokea juzi ni hatari na  kwamba linatishia usalama wa raia na mali zao.

Kuali ya THBUB

Kwa upande wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imesema imepokea kwa masikitiko na kulaani vikali tukio hilo.

Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti THBUB, Bahame Nyanduga, imeeleza kuwa mauaji hayo ya kikatili yametokea kwa askari polisi wasiokuwa na hatia waliokuwa kazini.

“Kumbukumbu zinaonyesha kuwa matukio ya mauaji ya askari polisi na wananchi wengine maeneo tofauti mkoani Pwani tangu mwaka 2015 yamekuwa yakiongezeka na kusababisha uvunjifu wa haki za binadamu, hususani haki ya uhai inayolindwa na Katiba ya nchi na madhara mengine kwa familia za wahanga, kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Alisema ikumbukwe kwamba, askari polisi wanapokuwa kazini wanatekeleza majukumu muhimu ya kulinda raia na mali zao, kwa hiyo usalama wao unategemewa na Watanzania wote.

Aliongeza yeyote yule anayewaua askari polisi si tu anataka kuwachonganisha askari polisi na raia, bali pia anawaweka raia hao katika hofu kubwa ya usalama na mali zao.

Alisema kutokana na hali hiyo, tume inashauri katika kuhakikisha kuwa haki ya kuishi ya askari polisi na wananchi wote inalindwa na Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla, wafanye uchunguzi wa kina ili kubaini sababu za mauaji haya kujirudia mkoani Pwani.

Alisema polisi wanapaswa kuhakikisha wahusika wote wanapatikana na wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake.

Kauli ya THRDC

Wakati huo huo Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini (THRDC),  umesema mauaji hayo yanatishia usalama wa wananchi na mali zao na endapo yataendelea usalama wao utakuwa shakani.

Akizungumza jijini jana Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema matukio yanayotokea ni dhahiri kuwa usalama wa wananchi kwa sasa ni mdogo kwa kuwa askari wanaouawa ni watu wenye uzoefu na weledi mkubwa katika kupambana na wahalifu.

“Ni dhahiri kuwa vitendo vya askari kuuawa kwa sasa vimeshamiri, kama askari wenye silaha kali za moto na mafunzo wanauawa kama  ndege na kuku nani atabaki salama, je, hawa wananchi ambao hawana mafunzo yoyote watabaki salama, hii hali ni wazi kuwa usalama wa wananchi hasa wa Pwani upo shakani,” alisema Olengurumwa.

Alibainisha kuwa hofu ya kuuawa  inaweza ikachangia utendaji kazi wa askari hao kushuka na hivyo kusababisha madhara zaidi.

“Zisipochukuliwa hatua kali za kiupelelezi na kubaini vichaka vya majambazi, kuna hatari kubwa kwa usalama wa nchi na raia wake, hadi sasa hakuna jitihada zozote zinazofanywa kuhakikisha askari hawaendelei kuuawa,” alisema Olengurumwa.

Alisema wahalifu wanaofanya matukio hasa ya kuua askari  na kuwapokonya silaha ambazo  hazijulikani wanazipeleka wapi endapo wataamua kuzitumia mitaani zinaweza kusababisha madhara makubwa.

Olengurumwa alisema kuanzia mwaka 2015 matukio ya uvamiizi yamekuwa yakijirudia bila kupatiwa ufumbuzi na hadi sasa yameshasababisha vifo vya askari polisi 30. 

“Zaidi ya askari polisi 30 wameuawa na bunduki aina ya SMG 60 za polisi zimepotea ama kuibiwa kutoka katika vituo kumi vya polisi kati ya 2015 mpaka 2017,” alisema Olengerumwa.

Alitoa baadhi ya orodha ya matukio hayo ni pamoja na lilitokea Januari 21, 2015 ambapo majambazi wenye silaha walishambulia Kituo cha Polisi Ikwiriri na kuua maofisa wawili na kuondoka na bunduki mbili ndogo za mashine.

Aliongeza kuwa Februari 2, mwaka huo huo katika Kituo cha Polisi Mngeta, Kilombero mkoani Morogoro, kilishambuliwa na bunduki aina ya SMG moja na magazine na makombora 30 zilichukuliwa.

Alilitaja tukio jingine kuwa ni lile la Februari 4, 2015 ambako ofisa mmoja G.7168 PC Joseph Swai, aliuawa Dodoma akiwa anafuatilia taarifa ya kiongozi wa Serikali za Mitaa ambaye alikuwa ameambatana naye akimpeleka kwa mtu aitwaye Tisi Sirii aliyekuwa akitaka kumuua mtoto wake wa miezi nane.

Olengurumwa aliongeza tukio jingine la mauaji ya askari lilitokea Machi 30, 2015 ambapo majambazi wenye silaha wanaotuhumiwa kuwa magaidi, walivamia katika Kituo cha Polisi cha St. Mathew Sekondari barabara ya Kilwa na kuua maofisa wa polisi wawili na kutokomea kusikojulikana.

Mei 29, 2015 pia ofisa wa polisi wa Kituo cha Polisi Tazara, alishambuliwa na majambazi wenye silaha ambao walichukua bunduki yake na kumwacha na majeraha.

Kwa mujibu wa Olengurumwa, katika tukio jingine Agosti 29, 2016 wakati Kikosi Kazi Maalumu cha Polisi kikiendelea na msako wa kufuatilia majambazi wenye silaha  mkoani Pwani, ofisa mmoja wa polisi, ASP Thomas Njuki, aliuawa.

Alisisitiza matukio ya kuuawa kwa askari yanatokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi hao ikiwemo  uwepo wa mazingira magumu ya kazi kuanzia makazi, vifaa hadi magari.

Kituo hicho kilitoa wito kwa Serikali  kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani kulichukulia jambo hilo kwa uzito mkubwa na kufanya uchunguzi ili kuweza kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua kali.

Kauli ya Chadema

Kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya askari wa Jeshi la Polisi wanane.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema, ilieleza kuwa taarifa hizo si tu kuwa ni za kuogofya bali pia ni za kuhuzunisha na kusikitisha hasa ikizingatiwa kuwa ni miezi michache tu iliyopita tukio la kihalifu kama hilo lilitokea maeneo hayo na Taifa kupoteza askari.

Alisema Chadema inatoa salamu za pole na rambirambi kwa IGP Mangu kwa msiba huo mkubwa ambao si tu kuwa ni pigo kwa Taifa bali ni mwendelezo wa matukio ambayo yanaashiria kuwa usalama wetu uko katika mtikisiko au mashaka makubwa .

“Tunamtaka IGP afanye uchunguzi wa kina na achukue hatua stahiki juu ya matukio yote ambayo yamekuwa yakihatarisha usalama wa raia na mali zao nchini kwa muda mrefu sasa ili  yaweze kukomeshwa mara moja, Watanzania hatujazoea matukio ya kihalifu kama yanavyoendelea kutokea nchini mwetu,” alisema Mrema.

Alisisitiza Jeshi la Polisi linatakiwa kujipanga upya ili kuzuia matukio kama haya kutokea ama kwa polisi wenyewe au kwa raia wengine kwa kuwa hilo ni jukumu lao la msingi.

Kauli ya ACT

Chama cha ACT Wazalendo kwa upande wake kimetoa wito kwa Watanzania kushikamana na vyombo vya ulinzi na usalama na kutoa ushirikiano kwao kuhakikisha matendo ya namna hii yanakomeshwa.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Kamati ya Amani na Usalama wa chama hicho, Mohammed Said Babu, chama hicho kilitoa pole kwa familia za maaskari hao.

“Tunachukulia kitendo hiki kama  shambulio dhidi ya Jamhuri na hatua kali na madhubuti zinapaswa kuchukuliwa, mlolongo wa matukio ya namna hii unaonyesha kuwa nchi yetu inapambana na kundi lisilo la kawaida na hivyo weledi wa hali ya juu unatakiwa katika kukabiliana na tishio hili dhidi ya Jamhuri yetu,” alisema Babu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles