24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge wataka mfumo wa elimu ufumuliwe

Hussein BasheNa Khamis Mkotya, Dodoma,

WABUNGE wameitaka Serikali kufanya mapitio makubwa ya mfumo wa elimu nchini ili kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya uchumi duniani.

Katika kutekeleza mpango huo, wabunge wamependekeza iundwe tume maalumu ya rais ya kitaalamu itakayofanya mapitio na kuangalia upya mfumo wa elimu ili kuondokana na matatizo yaliyopo katika sekta hiyo hivi sasa.

Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilitoa mapendekezo hayo bungeni jana, wakati inatoa maoni yake baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Tekonolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kuwasilisha hotuba ya bajeti yake.

Akisoma maoni hayo, mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alisema kamati imebaini changamoto nyingi katika sekta hiyo, hivyo suluhisho lililopo ni kufumua mfumo wa elimu uliopo sasa.

Bashe alisema baada ya tume hiyo kumaliza kazi yake, ripoti yake inapaswa kupelekwa bungeni ili Bunge nalo lijadili na kutoa mapendekezo kwa Serikali hususan ya sera na sheria  kuokoa elimu ya Tanzania.

“Kamati inashauri tume hiyo iangalie kuhusu sera za elimu, mfumo wa upatikanaji wa elimu, mfumo wa motisha kwa walimu, muda wa elimu ya msingi, sekondari na chuo kikuu; usimamizi wa elimu, uendeshaji na ugharimiaji wake,” alisema.

Akizungumzia hali ya elimu nchini, Bashe alisema: “Hali ya elimu nchini inasikitisha na ni hatari kwa usalama na uhai wa taifa letu. Tathimini na utafiti mwingi duniani umethibitisha kuwa elimu bora ni ile inayoweza kumsaidia raia kukabiliana na changamoto ili kujenga taifa imara na salama zaidi”.

UPINZANI

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeelezea kasoro na changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya elimu nchini, huku ikihoji sababu za Profesa Ndalichako kuvunja Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu  (TCU) siku moja kabla ya kusoma bajeti yake.

Msemaji wa kambi hiyo kuhusu wizara hiyo, Suzan Lymo, alisema Serikali imewatoa kafara wanafunzi 424 wa Chuo Kikuu cha Mt. Joseph ili kutengeneza mazingira ya bajeti ya wizara hiyo kupita kwa urahisi.

“Kitendo cha Waziri wa Elimu kuivunja bodi ya TCU jana (juzi) Mei 25, 2016 kutokana na kudahili wanafunzi wasiokuwa na sifa ya kujiunga na vyuo vikuu siku moja kabla ya mjadala wa hotuba yake, ni kujaribu kwa hila kulizuia Bunge kujadili kwa kina udhaifu mkubwa wa Serikali kupitia TCU katika kusimamia ubora wa elimu ya juu nchini,” alisema.

Awali akiwasilisha bajeti ya wizara yake, Waziri Ndalichako aliliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh trilioni 1.396 ili kutekeleza majukumu ya wizara hiyo kwa ufanisi.

Profesa Ndalichako alisema katika mwaka 2016/2017 wizara yake itaendelea na utekelezaji wa sera ya elimu na mafunzo ya 2014 na mikakati yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles