28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Meya Tanga aanza kuonja machungu

Mustafa SelebossNa Amina Omari, TANGA

MEYA wa Jiji la Tanga, Mustafa Seleboss, ameanza kuonja machungu ya kukataliwa hadharani na kususwa katika vikao vya maendeleo.

Tangu alipochaguliwa kushika wadhifa huo, amekuwa yuko kimya hasa baada ya madiwani wa Chama cha Wananchi (CUF) kuibua madai ya kuchakachuliwa kura zao, huku wakiamini aliyekuwa mgombea wao wa umeya, Rashid Jumbe, ndiye alikuwa mshindi halali.

Jana wenyeviti wa serikali za mitaa wa CUF walisusia kikao cha kutathimini shughuli za maendeleo kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa, Martine Shigellah, na kutoka nje huku wakiimba nyimbo za kutaka kuondolewa meya huyo ndipo  kikao hicho kifanyike.

Dalili za wajumbe hao kususia kikao hicho zilianza kuonekana mapema kabla ya kuingia mkuu wa mkoa.

Baadhi ya wenyeviti wanaotokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walikuwa katika vikundi wakijadiliana na kupanga mikakati yao.

Katika kikao hicho, Shigellah alikuwa amefuatana na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Abdallah Lutavi na Meya Seleboss.

Walipoingia ukumbini, wenyeviti hao zaidi ya 50 waliimba wimbo wa kutomtambua meya huyo na kutaka atolewe katika kikao hicho.

“Hatumtambui meya kikao siyo cha kwake kwa sababu  katika taarifa tulizozipata za kikao hiki hakutakiwa kuwapo, hivyo kama atashiriki sisi tutatoka nje ikizingatiwa uongozi wake si halali ni wa mizengwe,” alisikika mmoja wa wenyeviti hao akipaza sauti ndani ya ukumbi wa mikutano.

Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wenzake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Ngamiani Kusini, Omar Nassor,  alisema  waliamua kutoka nje ya ukumbi kwa sababu hawamtambui meya huyo kwa vile hakuchaguliwa halali.

Nassor alisema wasingeweza kushiriki kikao hicho hadi   meya huyo atakapotoka nje ya ukumbi huo.

“Tanga tunataka maendeleo, lakini viongozi wetu hawana nia ya kutuletea maendeleo, hivyo tunamuomba Mheshimiwa Rais Magufuli aje kutumbua majipu ya Tanga ya viongozi ambao wanakwamisha maendeleo kwa makusudi,” alisema Nassor.

Pamoja na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa Shigellah aligomea suala hilo na kuendelea na kikao hicho na wenyeviti wa CCM waliokuwa ndani ya ukumbi.

Alisema katu hatokuwa na msamaha na kiongozi yeyote atakayeleta siasa kwenye shughuli za maendeleo na kusababisha miradi ya maendeleo kukwama kwa sababu ya itikadi za vyama.

“Leo mna bahati nimewasamehe, lakini kama kitendo hiki kingefanyika katika maeneo yenu ya kazi lazima mngekiona ambacho ningewafanya,” alisema Shigellah.

Sambamba na hilo, aliwataka wenyeviti hao kuweka itikadi za vyama vyao pembeni ili kuweza kuharakisha maendeleo ya wananchi katika maeneo yao ikiwemo kuimarisha ulinzi na usalama.

Akizungumzia tukio hilo, Meya Seleboss alisema wao ndiyo wenye Serikali hivyo wapinzani tabia ya kususia ni jadi yao na hawawezi kushangazwa na kitendo hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles