23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge, wasomi wamchambua Majaliwa

IMGS0934VERONICA ROMWALD NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

SAA chache baada ya kuteuliwa kwa Waziri Mkuu mteule, Kassim Majaliwa, baadhi ya wabunge, wasomi na wananchi wa kawaida wamemchambua kiongozi huyo.

Wamesema  upya wake katika nafasi hiyo nyeti ya juu utasaidia kuleta mabadiliko ya kweli serikalini.

Mbunge wa Isimani, Wiliam Lukuvi (CCM),  alisema  Majaliwa amekuwa mtendaji mzuri na asiyechoka tangu alipokuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) anayeshughulikia elimu.

Alisema Rais Dk. John Magufuli  hakubahatisha kumteua Majaliwa na   ana imani atasimamia nafasi hiyo kwa uadilifu na usikivu mkubwa.

“Uteuzi wake si wa kubahatisha, waziri mkuu hateuliwi na magazeti na Rais Magufuli hashurutishiwi kuchagua.

“Kassim ni mwadilifu, mchapakazi, msikivu na kijana… tuna imani kwamba ataendana na kasi ya Rais Magufuli, yamesemwa mengi kwenye magazeti lakini huu ndiyo ukweli,” alisema.

Alisema wapo wengi wanaohoji kwa nini ameteuliwa akitokea katika ngazi ya Naibu Waziri.

Lukuvi  aliwataka Watanzania kukumbuka historia   ikizingatiwa Waziri Mkuu wa Serikali ya awamu ya tatu, Fredrick Sumaye aliteuliwa akitokea  nafasi ya Naibu Waziri.

“Watanzania wasiwe na wasiwasi na watambue kwamba viongozi wanaokuwa katika nafasi ya unaibu wanaifahamu zaidi nchi.

“Waziri Majaliwa ni mwalimu kitaaluma nafasi ambayo imemsaidia kujifunza mambo mengi,” alisema.

Sakaya

Mbunge wa Kaliu,a Magdalena Sakaya (CUF),  alisema Majaliwa ni kiongozi asiyekuwa na makundi hivyo ana imani   Watanzania watapata maendeleo wanayoyataka.

“Namfahamu Majaliwa tangu akiwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo nimefanya naye kazi kwa karibu.

“Alipoteuliwa kuwa waziri kwa kweli tulisikitika kwa sababu ni mchapakazi mzuri tena hana kashfa yoyote,” alisema.

Msigwa

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema hajafurahishwa na uteuzi wa Majaliwa ingawa ni mtu wake wa karibu.

Msigwa alisema hicho ni kielelezo  kwamba  Rais Magufuli ameanza vibaya.

Mwanahabari nguli nchini, Manyerere Jackton, alisema ana matarajio kwamba Majaliwa atafanya mambo makubwa ingawa watu wengi wanamuona kuwa kiongozi mkimya.

“Hata Sokoine hakuwa na makeke, hakuwa mtu wa kelele nyingi lakini kazi yake iliweza kuonekana.

“Hivyo nina imani kwamba Majaliwa atafanya kazi na kama akilegalega sidhani kama Rais Magufuli atamvumilia,” alisema.

Mandishi mwingine nguli, Dk. Gideon Shoo, alisema Majaliwa ni kiongozi mfuatiliaji.

Alisema na imani anazifahamu kero nyingi zinazowakabili watanzania kwa vile amefanya kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

“Ofisi ile najua imempa nafasi ya kutambua kero nyingi zinazowakabili watanzania kwa sababu amepata fursa ya kuzunguka katika maeneo mengi hivyo watanzania.

“Tunatarajia   hiyo itamuwezesha kuisimamia serikali vizuri,” alisema.

Wasomi

Wakizungumza na MTANZANIA kwa wakati tofauti Dar es Salaam jana  baadhi ya  wasomi   walisema upya wa Majaliwa Serikali utasaidia kuimarisha utendaji.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki cha  Ruaha mkoani Iringa, Profesa Gaudence Mpangala, alisema anashindwa kumuelezea kiongozi huyo kwa kuwa hamfahamu vizuri.

Alisema kuteuliwa kwa Majaliwa ni wazi Rais Dk. John Magufuli alipewa ushauri mzuri wa kupata mtendaji wa Serikali.

“Simfahamu vizuri Waziri Mkuu mteule Majaliwa (Kassim)… ila Rais Magufuli atakuwa anamfahamu zaidi.

“Kutokumfahamu  kwangu si tatizo kwa wengine   ingawa kwangu inaweza kuwa hivyo kwa kuwa tulizoea kupata kiongozi   anayejulikana,” alisema Profesa Mpangala.

Mhadhiri wa Uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja, alisema hamjui sana Majaliwa.

Alisema anachokifahamu kuwa ni mwadilifu na mchapakazi na   anayo sifa ya kuwa Waziri Mkuu.

“Anaweza kuwa kiongozi wa mfano kwani amepatikana tofauti na tulivyokuwa tunafahamu, hasa kati ya wale tuliokuwa tunawatarajia… matokeo yake  imekuwa tofauti,” alisema.

Aliyekuwa mgombea ubunge wa viti maalumu kupitia  CCM Mkoa wa Arusha, Violet Mfuko,  alisema ameupokea uteuzi   kwa furaha kutokana na uadilifu wa kiongozi huyo.

Alisema uteuzi wa Majaliwa ni miongoni mwa ahadi za Rais Dk. John Magufuli za kuleta mabadiliko  ya kweli katika kila eneo la nchi   na kurudisha amani.

“Uteuzi huo ni mfano wa Baraza la Mawaziri linalotarajiwa kukamilika hivi karibuni.

“Bado tunaona jinsi anavyoibua viongozi wapya ambao ni wachapakazi wazuri,” alisema Mfuko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles