27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge wamkosoa Maghembe

maghembeNa Arodia Peter, Dodoma

WABUNGE wamemkosoa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, wakisema miradi mingi aliyoisema katika hotuba yake haina uhalisia.

Wakichangia mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016, wabunge hao bila kujali itikadi zao za kisiasa, waliikosoa hotuba yake wakisema miradi mingi haitekelezeki.

Mbunge wa Viti Maalumu, Azza Hamad (CCM), aliikosoa kwa kuainisha kuwa vituo vya maji vinavyofanya kazi katika Kijiji cha Kagongwa, mkoani Shinyanga ni vinane tu badala ya 22 vilivyomo katika hotuba yake.

Alikitaja pia Kijiji cha Isaka, mkoani Shinyanga kuwa takwimu zake zimechakachuliwa katika hotuba ya Maghembe, aliyosema vituo vinavyofanya kazi katika kijiji hicho ni 53, wakati ukweli kuna vituo vitatu tu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje, alisema Maghembe hakuzungumza ukweli.

“Spika, robo tatu ya takwimu katika hotuba ya waziri sio za kweli, tumtake Maghembe aende akarekebishe takwimu zake aweke za kweli,” alisema Wenje.

Naye Mbunge wa Nkasi, Ally Keissy (CCM), alisema hawezi kuunga mkono bajeti hiyo kwa kuwa ni kiini macho.

Alisema Maghembe amekuwa akipokea takwimu zilizopotoshwa ambazo hazina utafiti wa kina na badala yake fedha za wizara zinaliwa na watumishi wa halmashauri pamoja na wizara.

Alisema katika jimbo lake la Nkasi kuna wizi na hujuma nyingi katika miradi ya maji, jambo alilosema ameshalitolea taarifa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), lakini hawajalifanyia kazi kwa sababu nao wanahongwa na watumishi wa Idara ya Maji na kusababisha kukwama kwa miradi yote ya maji.

Naye Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema), alisema ukosefu wa maji katika maeneo mbalimbali nchini unawapa wakati mgumu wabunge namna ya kuwaambia wapiga kura wao.

“Sisi wabunge tunakuja hapa kuishauri Serikali, tunataka ilete maji haisikii, sasa sijui tuwapige viboko humu ndani labda watasikia,” alisema Silinde na kusababisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, kusimama na kumwambia mbunge huyo kuwa kupigana ni kosa la jinai hivyo atashughulikiwa na sheria.

Naye Mbunge wa Rungwe Magharibi, Profesa David Mwakyusa (CCM), alimtaka Magembe asione aibu kuweka kipaumbele kwa ajili ya kutekeleza miradi ya zamani badala ya kuomba mipya ambayo haitekelezeki.

“Msisifike kwa sababu ya kuibua miradi mipya, bali msifike kwa kukamilisha iliyopo na waziri asione aibu kuleta bajeti kwa ajili ya kuomba fedha za kukamilisha miradi ya zamani ili kuondoa viporo,” alisema Profesa Mwakyusa.

MAONI YA KAMATI
Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, ilisema Serikali haina nia ya dhati ya kupunguza tatizo la maji nchini kutokana na kutoa asilimia 26 tu ya fedha za maendeleo za Bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015.

Ili kumaliza tatizo hilo, kamati hiyo imeitaka Serikali ihakikishe fedha itakayoidhinishwa na Bunge mwaka 2015/2016 inatolewa yote kwa wakati ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo mingi imekwama kutokana na uhaba wa fedha.

Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo, Mwenyekiti wake, Profesa Peter Msolla, alisema wizara hiyo iliidhinishiwa jumla ya Sh bilioni 488.8 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini hadi kufikia Machi mwaka huu, ilipokea Sh bilioni 129.3 .

TAARIFA YA UPINZANI
Akiwasilisha taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa Wizara ya Maji, Mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk Mohamed (CUF), alisema tatizo la maji nchini litaendelea kukua kwa sababu takwimu zinajionyesha wazi.
“Sekta ya maji inakabiliwa na upungufu wa watumishi 6,901 na pia ikumbukwe kuwa mikoa, wilaya na halmashauri zimeongezeka, huku watumishi wengine wakiwa wamestaafu. Takwimu za wizara zinaonyesha wataalamu wanaohitajika ni 8,749, lakini waliopo ni 1,848,” alisema Rajab.

PROFESA MAGHEMBE
Awali, akisoma hotuba yake kwa mwaka 2015/2016 ambayo ni Sh bilioni 458.9, alieleza jinsi Serikali ilivyotekeleza miradi ya kusambaza maji mijini na vijijini, likiwemo Jiji la Dar es Salaam.

Kuhusu miradi ya maji maeneo ya mijini, alisema katika mwaka 2014/2015, Serikali imetekeleza miradi hiyo katika mikoa saba ya Kagera, Musoma, Lindi, Kigoma, Sumbawanga, Mtwara na Babati na kufafanua maendeleo ya mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles