29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

JK: Rais ajaye ana kibarua kigumu

jkNa Mwandishi Wetu,
RAIS Jakaya Kikwete amesema rais ajaye atakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha Tanzania inaendelea kubaki kuwa moja kwa kudumisha umoja huo unaotokana na muungano wa nchi mbili.
Kikwete alitoa kauli hiyo siku chache baada ya makada wa chama hicho kuanza kuchukua fomu kuomba ridhaa ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Hadi sasa waliochukua fomu ni mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, kada wa chama hicho, Amos Siyantemi na Balozi Ally Karume.
Wengine ni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Steven Wasira, waliokuwa mawaziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Profesa Sospeter Muhongo.
Waziri wa Ofisi ya Rais Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani.
Taarifa iliyotolewa na Mwandishi wa Habari wa Rais, Premi Kibanga, aliyeko nchini Sweden ilieleza kuwa Rais alitoa kauli hiyo katika mkutano wake uliofanyika jijini Stockholm, alipokuwa akizungumza na Watanzania waishio humo mara baada ya kuwasili na kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia Juni 3 hadi 5, mwaka huu.
“Hapa tulipofikia lazima tuhakikishe Taifa linakuwa moja, kuna vyama na makabila mbalimbali, lazima tuhakikishe nchi inabaki moja,” alisisitiza Rais Kikwete.
Rais Kikwete alipokewa na Watanzania mbalimbali walioko nchini Sweden kwa ajili ya shughuli za kikazi, kimasomo na ambao wanaishi nchini humo.
Watanzana hao pia walimsomea Rais Kikwete risala ambayo pamoja na mambo mengine, walitaka kujua kuhusu haki yao ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu ujao.
“Suala hili linategemea Tume ya Uchaguzi, likiwekewa utaratibu linawezekana, kwa sasa taratibu zake hazijawekwa, lakini ninaamini kuwa uchaguzi ujao utakuwa wa mwisho kwa Watanzania wanaoishi nje kutopiga kura,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia alielezea matumaini yake kuwa Tanzania itapata kiongozi mzuri na kuelezea mafanikio ambayo serikali yake imeyapata na kutumaini kuwa yatadumishwa na kuendelezwa na Rais ajaye.
Awali akisoma risala ya Watanzania, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania nchini Sweden, Tengo Kilumanga, alimpongeza Rais Kikwete kwa kuridhia na kuonyesha nia ya dhati ya kumaliza kipindi cha uongozi wake na kuwa mfano bora katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tunakupongeza Mheshimiwa Rais, viongozi wengi katika Bara la Afrika huwa hawaagi, umefanya kitendo cha kishujaa sana.
“Viongozi wa Afrika huwa hawaagi kwa sababu siku ya kuondoka madarakani huwa haijulikani, hii inaonyesha wewe si mtu wa kupenda madaraka,” aliongeza Kilumanga.
Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Kikwete ya kuaga nchi wahisani na wenza katika maendeleo, ambapo alianzia katika nchi za Nordic.
Sababu kubwa za kuanzia katika nchi hizo inatokana na historia ya uhusiano wa nchi hizo kwa Tanzania tangu kupata Uhuru.
Rais Kikwete anaendelea na ziara yake nchini Sweden, ambapo anatarajia kufanya mazungumzo na wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali kwa lengo la kuwahamasisha kuja kuwekeza nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles