Katibu wa Bunge, Steven Kagaigai amesema nafasi za ubunge zilizoachwa wazi baada wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF) kufukuzwa uanachama, zilijazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria, na Wabunge waliopatikana kujaza nafasi hizo wanaendelea kutekeleza majukumu yao ya kibunge.
Amesema kumekuwapo na tafsiri isiyo sahihi ya uamuzi wa Mahakama inayotolewa na baadhi ya watu na vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii kusambaza taarifa potofu kwamba wabunge waliofukuzwa na CUF wamerejeshwa bungeni kwa uamuzi wa Mahakama baada ya kurejeshewa uanachama.
Katika taarifa yake aliyoitoa leo Novemba 30, Kagaigai amesema waliokuwa wabunge pia wameiandikia Ofisi ya Bunge wakiomba kufahamishwa utaratibu utakaotumika kuwarejesha bungeni.
“Ni vema ifahamike kuwa, hakuna sehemu yeyote katika uamuzi huo wa Mahakama inapoelezwa kuwa Wabunge hao wanatakiwa kurudishiwa ubunge wao.
“Uamuzi huo wa mahakama ni wa awali uliotolewa kwenye mapingamizi ya awali na uliwalenga walalamikiwa ambao ni Baraza la Wadhamini wa CUF pamoja na uongozi wake ambao uliamuru kuwa walalamikiwa wasitishe utekelezaji wa uamuzi wa kuwafukuza uanachama na kutojadili suala lolote kuhusu uanachama wa Walalamikaji hao hadi Mahakama itakapokamilisha kusikiliza shauri la msingi,” imesema taarifa hiyo.
Novemba 10, mwaka huu Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitoa uamuzi wa awali katika shauri lililofunguliwa na waliokuwa wabunge wanane wa Viti Maalumu CUF, lililofunguliwa kupinga uamuzi wa chama hicho kuwafukuza uanachama.