ARODIA PETER-DODOMA
WABUNGE wamekosoa mfumo na sera ya elimu ya mwaka 2014 wakidai ni kikwazo kwa maendeleo ya sekta hiyo nchini.
Wameshauri Serikali kufanya mabadiliko kwenye mfumo mzima wa elimu, vinginevyo taifa linatengeneza bomu la baadaye.
Wakichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, baadhi ya wabunge walisema iundwe tume maalumu kuchunguza suala la elimu Tanzania.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Shinyanga Mjini, Jumanne Kishimba (CCM) alisema elimu ya Tanzania haiwasaidii wahitimu badala yake wanabaki kuwa tegemezi na wavivu kwa sababu hawakuandaliwa sawasawa.
Kishimba pia alikosoa muda mrefu unaotumika kufundisha watoto hadi kuwa watu wazima kwamba unawafanya wengi kubaki wavivu hata wanapohitimu vyuo vikuu.
“Mheshimiwa mwenyekiti, suala la mfumo wa elimu tunayoenda nayo ni ‘bomu’ ndiyo maana Rais mstaafu Benjamin Mkapa amekuwa akilizungumza hili, lakini bado mko kimya.
“Elimu ya Tanzania ni kama kifungo cha maisha, kuanzia miaka 18 ya mtu kufanya kazi anakuwa shuleni hadi miaka 25, na akitoka huko na ‘degree’ (shahada) yake, hapati kazi, hajui kulima wala kufuga, na hiyo ‘degree’ hawezi kuweka bondi hata kupata mkopo benki wala ‘pharmacy’ (duka la dawa), ama anabaki kuwa tegemezi.
“Hivi ni utafiti gani wa kisayansi unaosema ubongo wa binadamu kila mwaka usome darasa moja? Kwanini tusifanye mwaka mmoja mtu asome madarasa matatu?” alihoji Kishimba na kuongeza:
“Hizi shahada wanazozisoma ni kama karatasi, zimejaa kila kona, hivi Serikali inaboresha elimu ipi kama hao inaowazalisha hawajafanyia kazi hicho walichokisoma?”
Mbunge wa Nkenge, Diodorus Kamala (CCM) alisema kwa mfumo uliopo sasa shule za msingi na sekondari nchini hazina mwenyewe kwa sababu haijulikani nani mwangalizi wake.
Alisema kwa mfano Waziri wa Elimu amejikita zaidi kwenye elimu ya vyuo vikuu na pale anapoelezwa changamoto za shule hizo hutupa mpira kwa taasisi nyingine.
“Ninashauri turudishe mfumo wa zamani ambapo shule hizo zilikuwa chini ya Wizara ya Elimu, lakini pia walimu tuwape stahiki zao ikiwamo kuwaheshimu,” alisisitiza mbunge huyo.
Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Lyimo (Chadema) alisema mfumo wa elimu wa mwaka 2014 umeanza kufanyiwa maboresho kabla ya kuanza kutumika jambo ambalo linadhihirisha kwamba haufai na haukushirikisha wadau wa sekta hiyo.
Lyimo pia alishauri fungu la fedha la Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu liwekwe peke yake na lisichanganywe na fedha za maendeleo kurahisisha ufuatiliaji.
Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) alishauri wabunge wote kuondoa tofauti zao wakati wa kujadili na kupitisha bajeti ya wizara hiyo ili kuokoa kizazi cha Tanzania.
“‘We must think big, think global’ namna gani tunakuza watoto wetu, namna gani tunawapa walimu wetu ambao ni walezi wakuu wa taifa letu waweze kuliangalia taifa, waweze kuwa na utulivu.
“Profesa Joyce Ndalichako dada yangu ulikuwa kwenye taasisi ya elimu, ulikuwa Baraza la Mitihani (NECTA), sasa umetoka huko umepewa dhamana hiyo unaacha ‘legacy’ ya namna gani kwa taifa la Tanzania kwamba umeanzisha mfumo huu unaiona Tanzania ya miaka 50, ya miaka 30 yenye uelewa wa hali ya juu,” alisema.