20.8 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Tunawatakia wafanyakazi Mei Mosi njema

Rais Dk. John Magufuli leo anatarajia kuwa mgeni rasmi katika sherehe za wafanyakazi (Mei Mosi) ambazo kitaifa zinafanyika mkoani Mbeya.

Katika sherehe hizo ambazo Watanzania huungana na wafanyakazi wengine duniani kusherehekea, huwasilishwa mambo mbalimbali yakiwamo ya kilio cha nyongeza ya mishahara.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Dk. Yahya Msigwa, anasema maandalizi ya maadhimisho hayo yamekamilika na wanategemea wafanyakazi na wananchi wa mkoa huo na mingine ya jirani watajitokeza kwa wingi.

Pamoja na mambo mengine, siku hii hutumiwa na wafanyakazi kwa maonesho mbalimbali ya kazi wanazofanya.

Kutokana na hilo, ni wazi leo Watanzania watajionea mambo mengi mazuri yanayofanywa na wafanyakazi hawa kila kukicha, ikiwamo bidhaa huduma na bidhaa wanazozalisha.

Tunaamini maandalizi ya mwaka huu yamekuwa mazuri, kwa sababu viongozi wa shirikisho wamekuwa na vikao vizito na Serikali juu ya kujadiliana mambo mbalimbali, lakini kubwa likiwa ni nyongeza ya mishahara ambayo wamekuwa wakiililia siku zote.

Pamoja na mapendekezo ya kiwango cha mshahara kwa wafanyakazi walichopendekeza kwa Serikali, hadi sasa wanalipwa Sh 375,000 kima cha chini kwa wale wa Serikali, wakati mapendekezo yalikuwa Sh  750,000, huku sekta binafsi wakilipa kuanzia Sh 100,000 kima cha chini.

Kwa hakika kiasi hiki ni kidogo kulinganisha na hali halisi ya kupanda kwa gharama za maisha kila siku, ni mategemeo yetu kwamba Serikali itakuja na majibu ya msingi katika suala hilo.

Tunasisitiza hili kwa sababu tunaamini Serikali hii ni sikivu kama ambavyo imekuwa ikisema, hivyo itaangalia namna ya kuboresha mishahara hii ili kwenda sawa na hali ya mwananchi wa kawaida.

Kuendelea kulipwa kiasi kidogo, kumesababisha wafanyakazi kuishi katika mazingira magumu, jambo ambalo tunasema umefika wakati wa kupatiwa ufumbuzi sasa.

Ni mategemeo yetu kuwa kamati maalumu ya kushughulikia mishahara iliyofanya utafiti ili kuangalia kima cha chini cha mshahara  itakuwa imekuja na majibu mazuri ambayo yatawasilishwa  mbele ya Rais Magufuli leo na yeye atayapatia ufumbuzi.

Kamati  hiyo ambayo ilifanya utafiti  kuhusiana na hali halisi ya maisha kwa sasa, kima cha chini cha mshahara wa mfanyakazi, kodi, pango,  nauli na mahitaji mengine, ilibaini mshahara wanaolipwa ni mdogo na hauwezi kukidhi mahitaji. Haya ni matatizo ambayo yanakwamisha juhudi za mfanyakazi kusonga mbele.

Pamoja na hali hiyo, Serikali imekuwa ikifanya mambo mengi mazuri kwa wafanyakazi hawa, ikiwamo kuendelea kupunguza gharama za kodi inayokatwa kwenye mishahara ambayo imekuwa kero kwa siku nyingi. Hii ni ahueni kwa mfanyakazi mwenye kipato cha chini.

Tunaamini hatua kama hizi ndiyo zimesababisha hata malalamiko mengi kuendelea kupungua kutoka kwa wafanyakazi siku hadi siku.

Sisi MTANZANIA tunaungana na wafanyakazi wengine kuwatakia kila heri Watanzania katika shehere za leo, huku tukisisitiza kwa nia njema kwamba kasoro ndogo ndogo za wafanyakazi hawa sasa umefika wakati wa kuzimaliza.

Kwa kuwa Rais Magufuli amekuwa na falsafa yake ya kutetea wanyonge, basi  wafanyakazi wanapaswa kuwa watulivu, tukiamini kilio chao kimefika kwa mwajiri wao na kwa wakati sahihi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles