27.7 C
Dar es Salaam
Monday, February 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge wahojiwa Takukuru

job* Ndugai atoa ufafanuzi wa tuhuma za rushwa

*Asema vyombo vya dola kufanya uchunguzi

*Kamati iliyosusa yaendelea na vikao Dar

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SIKU moja baada ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, kupangua wenyeviti na makamu wenyeviti kwa kuwaondoa kwenye kamati walizokuwa wanaziongoza, hatimaye Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), imewahoji wabunge watatu ambao wanatajwa kuhusika na mgawo wa fedha.

Uamuzi huo umekuja baada ya gazeti la MTANZANIA kuripoti hatua ya baadhi ya wabunge kuhongwa fedha na baadhi ya mashirika ya umma.

Taarifa kutoka ndani ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), zililiambia MTANZANIA kwamba tangu juzi baada ya kuripotiwa kwa taarifa hiyo maofisa wa taasisi hiyo wamekuwa na kibarua cha kuwahoji wabunge hao.

“Ni kweli tumewahoji wabunge watatu hadsi sasa kutokana na tuhuma za rushwa na suala hili tunalichukulia uzito wa pekee kwani Bunge ni mhimili unatakiwa kuwa safi.

“… siwezi kuwataja kwa sasa kwani hatua hii inaweza kuharibu uchunguzi wetu ambao kwa sasa upo katika hatua za awali na tunaamini tunaweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa na wale ambao watabainika tutawafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria,” alisema mmoja wa maofisa wa Takukuru ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Juzi Spika wa Bunge, Job Ndugai, alifanya mabadiliko ya baadhi ya wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge huku akiwaondoa wenyeviti na makamu wevyeviti watano katika kamati walizokuwa wakiziongoza.

Katika mabadiliko hayo yaliyowagusa jumla ya wabunge 27, Spika Ndugai, ametoa maelekezo ya kujazwa kwa nafasi zilizoachwa wazi za wenyeviti na makamu wenyeviti walioguswa na panga pangua hiyo na kusititiza utekelezaji wa maagizo yake kuanza mara moja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ofisi ya Bunge, Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano ya Umma, uamuzi wa  Spika umezingatia mahitaji mapya na changamoto zilizojitokeza baada ya kuundwa kwa Kamati za Bunge hapo Januari mwaka huu.

Taarifa hiyo ilieleza kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa Spika ya kuteua wabunge na kuunda kamati za Bunge, alizingatia kanuni ya 116 (3) ya kanuni za kudumu za Bunge kuwaondoa viongozi watano wa kamati na kwamba kamati ambazo zitaathirika na uamuzi wake zitapaswa kufanya uchaguzi wa viongozi walioondolewa kwa mujibu wa kanuni ya 116 (10) ya kanuni za kudumu za Bunge.

Wenyeviti walioguswa la rungu la mabadiliko yaliyofanywa na Spika Ndugai ni Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCN) ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini aliyehamishiwa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira,  Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), ambaye alikuwa Mwenyekitiwa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji (PIC), aliyehamishiwa kamati ya Katiba na Sheria.

Mwingine ni Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Mary Mwanjelwa (CCM),  ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ambapo amejikuta akihamishiwa kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Makamu wenyeviti walioondolewa kwenye kamati zao ni Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), ambaye aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Sambamba na hao, wabunge wengine 22 nao wamehamishwa kutoka kamati walizokuwa kwenda katika kamati nyingine.

Taarifa za Bunge ambazo gazeti hili limezipata zimeeleza kuwa mabadiliko hayo yamelenga kuwaondoa waliokuwa wakilalamikiwa kuhusu mienendo yao ya kikazi kwenye kamati walizokuwa, huku wengine wakihamishwa kwa ajili ya kwenda kujenga taswira mpya ya kamati zinazonyooshewa vidole.

MTANZANIA lilikariri taarifa za kibunge zilizoeleza kuwa taasisi zilizofikiwa na wabunge wanaotuhumiwa kuombwa rushwa kuwa ni Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

Ndugai afafanua

Jana Spika Ndugai, alitoa ufafanuzi katika Kituo cha Redio cha Clouds FM, wakati akizungumzia suala la kujiuzulu kwa wajumbe wawili na tuhuma za rushwa.

Alisema wao kama Bunge suala hilo wataliachia mamlaka zenye dhamana ya kuchunguza tuhuma hizo na uchunguzi ukikamilika taarifa zitatolewa.

“ Nimepokea barua za wabunge wawili wa kamati ambao wameomba kujiuzulu nimeshangazwa na kujiuzulu kwao kwa kuwa wao hawajatuhumiwa… nitazipitia barua zao na kuzitolea majibu,”alisema Ndugai.

Alisema jana wangewaita wabunge hao ili kuweza kusikiliza hoja zao  na wao kama Bunge hawafanyi uchunguzi wowote kuhusu hali hiyo.

“Sisi kama Bunge hatufanyia uchunguzi wowote dhidi ya mbunge yoyote kwa sasa ila vyombo vya dola vinaweza kuwa na utaratibu huo sasa au baadaye kidogo.

“Hata wakichunguza hawaripoti kwa Spika ila tunawaomba Watanzania wazidi kuwa na imani na Bunge lao na watuombee na tunaamini Bunge la 11 litawafanyia kazi vizuri,” alisema Spika Ndugai.

Alisema suala la mabadiliko ya kamati ni la kawaida kama ilivyo kwa timu ya mpira kwa lengo la kuimarisha timu.

Makosa ya kususia vikao

Baada ya taarifa hizo aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Dk. Chegeni naye juzi aliwasilisha dokezo la kamati yake ofisini kwa Spika lililoeleza kuwa kamati yake iliyokutana jana katika ukumbi wa Saadan uliopo jengo la LAPF, Kijitonyama baada ya kumaliza majukumu yake ya kibunge ilijadili tuhuma za rushwa ilizoelekezewa.

Dokezo hilo lilieleza kusikitishwa na tuhuma hizo na kwamba wajumbe waliazimia kulitaka Bunge kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo na kwamba kuanzia jana wanasitisha kufanya kazi yoyote ya kamati hadi uchunguzi utakapokamilika.

Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Ofisi ya Bunge, Owen Mwandumbya, alisema ni kosa kisheria  wabunge kusitisha shughuli za Kamati za Bunge bila idhini ya Spika.

Mwandumbya  aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa ufafanuzi kuhusu  Kamati ya  Huduma  na Maendeleo ya Jamii kulitaka Bunge kufanya uchunguzi wa tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wenyeviti wa kamati mbalimbali ambapo tuhuma hizo zilisababisha wenyeviti kusimamishwa wadhifa huo hali iliyoifanya kamati hiyo kudai kuwa watasitisha shughuli za kamati kuanzia juzi

Mwandumbya, alisema mwenye mamlaka ya kusitisha vikao vya Kamati ya Bunge ni Spika pekee yake kwa mujibu wa sheria  huku akielezea kazi za mbunge kuwa ni pamoja na ushiriki wa vikao vya kamati.

“ Mbunge yoyote moja ya majukumu yake ni kushiriki kwenye kamati …hivyo kitendo cha kusitisha vikao bila idhini ya spika ni kosa kisheria,” alisema Mwandumbya.

Alisema pamoja na hali hiyo kamati hiyo jana iliendelea na shughuli zake kama kawaida na waliongozwa na mwenyekiti wa muda, hivyo hakuna taarifa walizopata za kusitisha kikao.

Alisema kuhusu suala la Mbunge wa Kigoma Mjini ,  Zitto Kabwe (ACT- Wazalendo) na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), kuandika barua za kujiuzulu ili kupisha uchunguzi dhidi ya wenyeviti wanaotuhumiwa kwa rushwa alisema Spika Ndugai,  amepokea barua zao na atazitolea majibu.

“Spika amepokea barua zao atatoa majibu na mbunge anayesusia shughuli za kamati anakaidi shughuli halali za Bunge ,”alisema Mmwandumbya.

ACT-Wazalendo na uchunguzi

Nacho Chama cha ACT-Wazalendo kimesema uamuzi wa kuwahamisha kamati viongozi na wajumbe wa kamati zilizotuhumiwa kupokea rushwa hautoshi.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kuhusu uamuzi wa Spika wa Bunge kufanya mabadiliko ya baadhi ya wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na Serikali za Mitaa, Yeremia Maganja, alisema kuwa ACT- Wazalendo haikubaliani na uamuzi huo kutokana na kuwa kufanya hivyo ni sawa na kuendeleza utamaduni mbovu.

Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge ndiyo chombo kikuu chenye madaraka kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake katika utekelezaji wa majukumu yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles