Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
Wabunge 47 na viongozi wa dini 14, wametajwa kuwa miongoni mwa wanaume waliotelekeza wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wanawake 480 waliofika katika ofisi yake jana, kati yao 47 wamesema wametelekezwa na wabunge huku 14 wakieleza wametelekezwa na viongozi wa dini.
Makonda amesema hayo leo Jumanne Aprili 10, alipokaribishwa kutoa salamu za mkoa, mbele ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla ya uzinduzi wa chanjo ya saratani iliyofanyika katika viwanja vya Mbagala Zakhiem, Temeke jijini hapa.
“Wengine wamewataja wafanyabiashara mashuhuri ambao ukiwatazama huwezi kuamini kama wanafanya ukatili huu,” amesema.
Amesema takwimu zinaonesha katika mwaka 2017, walizaliwa jumla ya watoto 129,347 na kwamba asilimia 60 wametelekezwa huku katika kituo kimoja kilichopo Wilaya ya Kinondoni pekee wanatunzwa watoto 274 ambao waliokotwa.
“Watoto hao waliokotwa wakiwa wametupwa kwenye mifuko ya rambo kama takataka, kina mama hawa wanateseka kulipa kodi, kununua chakula cha familia na mambo mengine.
“Kisha wengine wanasema Makonda nahusikaje humu wakati haya ni mambo ya Ustawi wa Jamii, sisi tunaendelea na nimeongeza siku za kuonana na kinamama hao,” amesema.