Na Mwandishi Wetu
UBALOZI wa Marekani nchini umesifu kazi zinazofanywa na Shirika la Vijana Nchini (Tayoa), katika kuwainua na kuwahamasisha vijana kujikwamua kiuchumi na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dk. Inmi Patterson, wakati ujumbe wa wabunge watano wa Bunge la Congress la Marekani wakiwa na familia zao, ulipotembelea ofisi za Shirika hilo zilizoko Bahari Beach, Dar es Salaam.
Wabunge hao wa Congress walioambatana na Kaimu Balozi wa nchi hiyo ni pamoja na Carly Paul, Bob Goodlatte, Steve King, Blake Farenthold, Mike Bishop na Sheila Jackson Lee.
Wabunge hao walijionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Shirika hilo ikiwemo elimu ya bure kuhusu masuala ya Ukimwi kupitia simu za bure, ujasiriamali na miradi mbalimbali ya kuinua vijana.
Balozi alisema yeye na ujumbe wake wamefurahi kuona kazi kubwa zinazofanywa na Tayoa kwa kushirikiana na taasisi za Marekani kama Kituo cha Kudhibiti Maradhi cha Center for Disease Control (CDC).
“Tumefurahi sana kuona kazi zenu na hasa mnavyowashirikisha vijana katika kujikwamua kiuchumi na kutafuta maendeleo, nawapongeza sana Tayoa kwa kazi kubwa mnayofanya,” alisema balozi.
Alisema Tanzania na Marekani zimekuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa muda mrefu ambao umekuwa ukiimarika mwaka hadi mwaka na kuahidi kuwa Serikali hizo mbili zitaendelea kushirikiana.
“Inafurahisha sana kuona vijana ambao wanaelimika kupitia vijana wenzao kama wanavyofanya Tayoa, vijana ambao wako tayari kushirikiana na wenzao kuleta maendeleo yao wenyewe na maendeleo ya Taifa lao,” alisema.
Mmoja wa wabunge hao, Sheila Jackson Lee, alisifu ubunifu ulioonyeshwa na shirika hilo katika kutekeleza miradi mbalimbali ukiwemo wa kutoa elimu bure kuhusu ugonjwa wa Ukimwi kupitia simu za bure.
“Mkurugenzi wa Tayoa, Peter Masika na Mwenyekiti wa Bodi ya Tayoa, Balozi Charles Sanga mmefanya kazi kubwa sana, mmetumia muda wenu mwingi kusaidia maendeleo ya vijana, hii kazi mnayofanya si kwa manufaa ya Watanzania tu bali dunia nzima,” alisema mbunge huyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tayoa, Peter Masika, alisema wabunge hao wamekuja kuangalia kazi zinazofanywa na Shirika hilo na namna wanavyotumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kuelimisha vijana masuala mbalimbali ikiwemo Ukimwi kwa njia ya simu bila malipo.