26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

UVCCM YAONYA SIASA KUCHANGANYWA NA DINI

Na Mwandishi Wetu -PEMBA

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umelaani hatua ya baadhi ya vyama vya upinzani nchini vinavyoeneza siasa chafu kwa kutumia mgongo wa dini kisiwani Pemba.

Kutokana na hali hiyo, umesema kuwa vyama hivyo vinahitaji kuepukwa na wananchi wapenda umoja kwa madhara ya kuchanganya dini kwenye siasa kwani ni jambo la hatari kwa nchi na watu wake.

Onyo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambapo alijionea baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu waliodai kubaguliwa kwenye nyumba za ibada tangu ulipomalizika Uchaguzi Mkuu visiwani humo.

“Mwanasiasa usitegemee kupata madaraka kwa kutumia siasa chafu za kuwagombanisha wananchi kwa sababu za dini, ukabila au kuwabagua kwa rangi na nasaba zao. Wanasiasa waliotoa maelekezo haya ni wazi wategemee kulipwa dhambi ya jasho hilo haramu,” alisema.

Shaka alisema ndiyo maana baadhi ya viongozi wakorofi katika upinzani huvunja Katiba za vyama vyao na kufukuzana wenyewe kwa wenyewe, hali inayochangia  kuwaponza baadhi ya wabunge wa Viti Maalumu kuvuliwa nyadhifa zao.

Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM alisema CCM itaendelea kurithi na kufuata kwa vitendo sera za vyama vya TANU na ASP ambavyo vilipiinga ubaguzi wa rangi, dini, ukabila kwa kukataa mwendelezo wa siasa za nasaba na uzawa.

“Wanasiasa wanaotegemea kupata urais kwa kuwagawa wananchi kwa imani za dini wataendelea kusota katika benchi kusubiri mpaka watakapokwendea mikongoja, hawatoshi kuwa viungo katika jamii,” alisema.

Muumini mmoja miongoni mwa waliofukuzwa kusali misikitini kwa sababu za kisiasa, Hafidh Hashim Mattar,  alisema wapo wanasiasa wa upinzani ambao huwaita wenzao ni madhalimu huku wakisahau kauli hizo huwa ni dhima kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

“Tumefukuzwa na kubaguliwa kwa sababu za kisiasa, kujengwa kwa msikiti huu umekuwa ni ukombozi kwa wafanyao ibada kwa ajili ya kumtii Mungu na si kuwafuata wanasiasa na viongozi wao,” alisema Hashim.

Hashim alisema misikiti si ofisi ya Tume ya Uchaguzi inayoteua wagombea, kutangaza siku ya uchaguzi au hata kuhesabu idadi ya kura za wagombea bali ni nyumba maalumu za ibada ambazo humwezesha mtu kuwasiliana na muumba wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles