24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE CCM WAMWOKOA HALIMA MDEE

Na MAREGESI PAUL-DODOMA


WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana walimwokoa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), asitumikie adhabu ya kutohudhuria vikao vya Bunge vilivyobaki katika Bunge la Bajeti linaloendelea mjini hapa.

Tukio hilo lilitokea baada ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kuwasilisha taarifa yake kuhusu baadhi ya wabunge na viongozi wa Serikali iliokuwa imewahoji baada ya kulidharau Bunge na mamlaka ya Spika.

Taarifa hiyo iliwasilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almas Maige (CCM).

Mbali ya Mdee ambaye alituhumiwa kumtukana Spika, Job Ndugai, wengine waliohojiwa na kamati hiyo ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema), Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti.

 Wakichangia taarifa ya kamati hiyo, wabunge wa CCM walisema kwa nyakati tofauti, kwamba pamoja na Mdee kufanya makosa na kutakiwa kutumikia adhabu hiyo, anastahili kusamehewa kwa kuwa alikiri kosa mbele ya kamati na pia aliomba msamaha bungeni akionesha kukiri kosa alilofanya.

KANGI  LUGOLA

Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM),  alisema Mdee alistahili kusamehewa kwa sababu alikiri kosa na kuomba msamaha tangu alipohojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

“Kitendo cha Halima Mdee kuomba msamaha huku akimtanguliza Mungu, kinatakiwa kuangaliwa kwa umakini wa hali ya juu kwa sababu inaonekana alijutia kosa lake.

“Wakati nikimwombea msamaha Halima Mdee, naomba pia Esther Bulaya aondolewe ile adhabu ya karipio aliyopewa na kamati,” alisema Lugola.

SERUKAMBA

Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba, alisisitiza umuhimu wa Mdee na wenzake hao kusamehewa kwa kuwa waliomba msamaha baada ya kukiri makosa yao dhidi ya Bunge na Spika.

Kwa mujibu wa Serukamba, kama Bunge litamsamehe Mdee na wenzake, litakuwa jambo jema kwa kuwa litaonesha ni kwa jinsi gani lilivyo makini katika utendaji wa kazi.

HAWA GHASIA

Kwa upande wake, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia, alisisitiza umuhimu wa watuhumiwa hao kusamehewa, lakini akataka Mdee alithibitishie Bunge, kwamba hatarudia kumtukana Spika pamoja na kulidharau Bunge.

“Pamoja na hayo, nawaomba wabunge wenzangu wanawake tuendelee kumsaidia Mdee ili asiendelee kuvunja kanuni za Bunge,” alisema Ghasia.

BULEMBO

Naye Mbunge wa Kuteuliwa, Abdallah Bulembo, alianza kwa kumpongeza Mbowe baada ya kukiri kosa mbele ya kamati ya Bunge huku akitaka Mdee na wenzake wasamehewe kwa sababu nao walikiri makosa yao mbele ya kamati hiyo.

Pamoja na hayo, alitaka Bunge liandae utaratibu wa kuwaadhibu wabunge wanaofanya makosa kwa zaidi ya mara moja.

JANETH MBENE

Mbunge wa Ileje, Janeth Mbene, pamoja na kuunga mkono Mdee na wenzake wasamehewe, aliwataka wabunge wawe na kawaida ya kujiheshimu kabla hawajaheshimiwa.

SIMBACHAWENE

Katika mchango wake, George Simbachawene ambaye pia ni Waziri wa Tamisemi, pamoja na kuunga mkono msamaha huo, alisema kuna haja kwa kanuni za Bunge kuboreshwa zaidi ili kuwabana zaidi wabunge wanaofanya makosa kwa zaidi ya mara moja.

 “Kwa hiyo, lazima sasa wabunge tunapokuwa tunaongea, tuwe na tahadhari kwa sababu matokeo ya huu mjadala yanatokana na baadhi yetu kukiuka kanuni na taratibu zetu kwa makusudi,” alisema Simbachawene.

Kwa upande wake, Mhagama ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye ulemavu, aliwapongeza Mdee na wenzake kwa jinsi walivyoonyesha ushirikiano mbele ya kamati hiyo ya Bunge.

Pamoja na hayo, alitumia kanuni ya Bunge ya 57 (1), kubadili mapendekezo ya kamati hiyo ya Bunge akitaka yaongezwe maneno yatakayolipa Bunge nguvu ya kumwadhibu Mdee bila kuishirikisha kamati pindi atakapokiuka kanuni za Bunge kama alivyozoea.

“Kanuni ya 57 (1) inataka hoja inayoletwa hapa, ibadilishwe kwa hoja nyingine itakayowasilishwa. Kwa hiyo nawasilisha kwamba, Halima Mdee akirudia tena kufanya kosa kama hilo, aadhibiwe bila kamati kukaa.

“Lakini pia, msamaha huu unaotolewa hapa, usiwe kigezo cha kuendelea kuvunja kanuni,” alisema Mhagama.

Baada ya hoja hiyo, Bunge liliridhia kusamehewa kwa Mdee, lakini kwa mujibu wa nyongeza ya kanuni iliyotolewa na Mhagama, iwapo mbunge huyo atafanya kosa jingine ataadhibiwa moja kwa moja na kiti bila kupelekwa kwenye kamati.

Wakati wabunge hao wakisema hayo, wabunge wa upinzani, Joseph Selasini wa Rombo kupitia Chadema na Riziki Ngwali wa CUF, nao walitaka Mdee asamehewe kwa kuwa alikiri kosa mbele ya kamati na pia Aprili 25 mwaka huu, alimwomba msamaha Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Awali, Maige aliyataja makosa ya Mbowe kuwa ni kutoa maneno ya utovu wa nidhamu kwa kudharau mamlaka ya Spika na kutoa maneno ya kuudhi kwa wabunge wengine wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, mwezi uliopita.

Kuhusu Mdee, alisema naye wakati wa mchakato wa uchaguzi wa wabunge hao, alitoa lugha ya matusi na ya kuudhi dhidi ya Spika Ndugai.

Kwa upande wa Bulaya, Maige alisema Mei 30, mwaka jana, mbunge huyo alifanya vurugu bungeni kwa kurusha ovyo vitabu na makaratasi wakati Wizara ya Maji na Umwagiliaji ilipokuwa ikihitimisha hoja yake ya bajeti ya mwaka huo.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisema alilidharau Bunge Februari mwaka huu kwa kusema wabunge wana kazi ya kusinzia bungeni wakati Mnyeti alidaiwa  kusema wabunge hawajielewi na anawashauri wafanye kazi zao na zingine waachie wengine wanaohusika nazo.

Wakati huo huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alieleza jinsi alivyopigiwa simu na mama yake Mdee alitaka wakutane juu ya tabia ya mbunge huyo.

Hata hivyo, alisema alikataa kukutana na mama huyo kwa kuwa aliamini suala hilo litamalizwa na Bunge kwa kufuata taratibu zilizopo. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles