Na MAREGESI PAUL-DODOMA
WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameapa kukwamisha Bajeti ya Wizara ya Kilimo, baada ya kudai kudharaulika kwa bei ya pamba.
Wakichangia bajeti ya Wizara ya Kilimo bungeni jijini Dodoma jana, ambapo wa kwanza alikuwa Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa (CCM), ambaye aliwahamasisha wabunge wanaotoka katika mikoa inayolima pamba, wasiunge mkono bajeti hiyo.
Kauli hiyo ya Ndasa, iliitoa alipokuwa akichangia bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/19 iliyowasilishwa na Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba.
“Kwanza kabisa nasema siungi mkono bajeti ya wizara hii kwa sababu haionyeshi namna ya kuwakomboa wakulima wa pamba katika nchi hii.
“Lakini pia, hivi ni kwanini bei ya pamba kila mwaka inalalamikiwa kutokana na kutoipandisha kama inavyotakiwa?
“Katika zao la pamba, wakulima wanalazimishwa kulipa madeni ambayo hayawahusu, hivi wakati madeni hayo yanakuwapo, hao wakuliwa walikuwepo?
“Katika bei ya pamba, wakulima wanakatwa shilingi mia moja kwa kila kilo moja, kwa hiyo, naomba hiyo shilingi mia moja mnayowakata, muirudishe na nawaomba wabunge wenzangu mnaotoka katika mikoa inayolima pamba, tuungane kuipinga bajeti hii hadi hapo Serikali itakapotwambia ni lini itairudisha ile shilingi mia moja wanayowakata wakulima na ni lini itapandisha bei ya pamba,” alisema Ndassa.
MASHIMBA
Baada ya Ndasa kuyasema hayo, Mbunge wa Maswa Mgharibi, Mashimba Ndaki (CCM), naye aliungana na mbunge mwenzake huyo na kusema haungi mkono bajeti ya wizara hiyo kutokana na madhara wanayopata wakulima wa pamba.
Kwa mujibu wa Ndaki, bei ya pamba mwaka jana ilikuwa ni Sh 1,200 kwa kilo, lakini mwaka huu imeshuka hadi Sh 1,100, jambo ambalo alisema haliwezi kukubaliwa na wakulima wa zao hilo.
“Mheshimiwa mwenyekiti, kule kwetu pamba ni siasa kwa sababu inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja na kibaya zaidi, baada ya msimu wa pamba kufunguliwa hivi karibuni, hadi sasa hakuna pamba iliyonunuliwa kutokana na mazingira mabovu ya ununuzi.