HANOI, VIETNAM
NDEGE ya Urusi ambayo ina shehena ya tani 40 za mizigo ya misaada ya kibinadamu, imewasili nchini Vietnam kuwasaidia waathirika wa kimbunga kilicholikumba taifa hilo hivi karibuni.
Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Misaada ya Mambo ya Dharura, ndege hiyo iliwasili juzi katika Uwanja wa Ndege mjini Cam Ranh, ikiwa ni baada ya Rais Putin kuiagiza Serikali yake kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha waathirika hao wanapata msaada.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa miongoni mwa shehena iliyomo ndani ya ndege hiyo ni mahema, vyakula, maziwa, makopo ya nyama na samaki.
Kimbunga hiyo aina ya Damri kiliyakumba maeneo ya katikati mwa Vietnam mwishoni mwa wiki na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 60 na kujeruhi wengine kadhaa.
Mbali na kusababisha vifo na majeruhi, pia majengo yapatayo 80,000Â yaliharibika na watu 40,000Â wameokolewa huku baadhi ya maeneo katika nchi hiyo yamebaki bila umeme.