New York, Marekani
FAMILIA za watu waliokufa katika mashambulio ya ugaidi Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani zimefungua mashtaka dhidi ya Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa gazeti la Marekani la USA Today, familia za watu 850 waliouawa na 1500 waliojeruhiwa katika mashambulio hayo zimefungua mashtaka katika mahakama ya Manhattan, New York.
Gazeti hilo limeandika kuwa Mahakama moja ya Marekani inautambua utawala wa Saudi Arabia kuwa uliwasaidia baadhi ya magaidi waliofanya mashambulio hayo.
Katika mashtaka hayo pia yametajwa majina ya maofisa wa serikali ya Saudi Arabia ambao walikuwa wakiwasiliana na magaidi katika miji ya Los Angeles, San Diego, Sarasota, Washington DC na Virginia miezi 18 kabla ya kutekeleza mashambulio hayo kwa kutumia ndege zilizotekwa nyara.
Baada ya mashambulioya Septemba 11 mwaka 2001 Bunge la Marekani liliunda kamati ya kuchunguza mashambulio hayo.
Ripoti hiyo ilitayarishwa na kuchapishwa lakini hadi sasa sehemu inayohusiana na Saudi Arabia ni siri.