Hadija Omary, Lindi
Mahakama Kuu Kanda ya Lindi, Jamii ya Watu wa Kusini (SEDO) na wadau wengine wa maendeleo wametoa fedha taslimu na vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 8,637,000 kwa waathirika wa mafuriko mkoani humo.
Misaada huyo imetolewa leo Jumapili Februari 9, kwa nyakati tofauti na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa huo Godfrey Zambi.
Misaada hiyo ni fedha taslimu Sh milioni 3.1 zilizotolewabna Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Nguo mifuko tisa, mabati 250 yenye thamani ya Sh milioni nne na unga viroba 15 vyenye ujazo wa kilo 25 na sukari mifuko nane ya kilo 25 vyenye thamani ya Sh 537,000 kutoka SEDO.
Akikabidhi msaada huo Jaji Mfawidhi Mahakama hiyo, Jaji Paul Gwembe amesema fedha hizo walizokabidhi ni michango kutoka kwa watumishi wa Mahakama zote za Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Nayebmwenyekiti wa SEDO, Brigedia Jeneral mstaafu, Aloyce Mwanjile pamoja na kutoa pole aliupongeza uongozi wa mkoa huo kwa namna walivyoshughulika na maafa hayo pamoja na kuwaokoa wananchi.
Akipokea misaada hiyo , Zambi aliwashukuru wadau hao kwa misaada waliyoitoa kwa ajili ya waathirika huku akiwatoa hofu kuwa misaada hiyo ipo katika mikono salama na itatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.