KINSHASA, Congo DRC
WATU 25 wameuawa katika mashambulizi mawili yanayoaminika kutekelezwa na kundi la waasi la Allied Democratic Forces, ADF, katika Mji wa Beni,uliopo Mashariki mwa nchi hii.
Mwandishi wa Sauti ya Amerika (VOA) aliripoti juzi kuwa idadi ya waliouawa eneo la Mangolikene, nje kidogo ya mji wa Beni, Kivu kaskazini, imeongezeka na kufikia 20.
Mwandishi huyo alisema kuwa watu wengine watano waliuwawa katika kijiji cha Paida kilichopo karibu na mji huo wa Beni.
Mwandishi huyo aliyepo mjini Goma alieleza kuwa mashambulizi hayo yalitokea usiku wa kuamkia Ijumaa.
Alisema kuwa nyumba kadhaa zilichomwa moto na kuna taarifa kwamba baadhi ya watu wametekwa nyara na kikundi cha watu waliowashambulia.
Alisema kuwa raia haoa wanasema kuwa waliowashambulia walikuwa wamevalia sare za kijeshi na walikuwa wanazungumza lugha ya Kilingala.
Msemaji wa jeshi katika eneo hilo, Kapteni Mak Hazzukay, alisema kwamba mauaji yametokea baada ya waasi kushambulia kambi ya jeshi.
Serikali ya DRC imekuwa ikilaumu kundi la ADF kwa mauaji, wizi wa kitumia nguvu na utekaji nyara, lakini wakati mwingine taarifa kamili hukosekana kuhusu wanaofanya mashambulizi.
Kundi la ADF, kutoka Uganda, limeuwa mamia ya watu tangu mwaka 2014.
Mashambulizi haya ya sasa yanajiri siku moja baada mgombea wa Urais, Martin Fayulu, mmoja kati ya wagombea wengine wa urais, kuzindua kampeni zake katika mji wa Beni.