NA KULWA MZEE , MOROGORO
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro,Elizabeth Nyembele, amewataka waandishi wa Habari za Mahakamani kufikisha taarifa sahihi kwa jamii.
Nyembele, ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano ya Waandishi wa habari za Mahakamani.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania, yanashirikisha waandishi na Wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya Habari.
Nyambele alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa Waandishi kwani yatawaongezea uelewa wa shughuli za Mahakama.
Alisema watajua hatua zinazofikiwa katika kesi na maboresho yanayofanywa na Mahakama.
Alisema kuna changamoto ya mashahidi kufika Mahakamani kwa wakati, jambo ambalo linasababisha mashauri kuchelewa kumalizika.
“Mpango wa Mahakama ni kumaliza mashauri kwa wakati, lakini bado kuna baadhi ya wadau hawajajua hilo…. Sisi tunakwenda mbio, wao wanatambaa.
“Mashahidi bado ni kikwazo hali inayochangia kuonekana mashauri yanachukua muda mrefu mahakamani, tunaomba wadau watupe ushirikiano tuweze kumaliza mashauri kwa wakati, “alisema.