33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

VYUO VISIFANYE MAKOSA KUDAHILI WANAFUNZI WASIO NA SIFA

Na LEONARD MANG’OHA

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imebadili mfumo wa udahili wa wanafunzi uliokuwa chini yake na sasa unafanywa na vyuo husika kuanzia mwaka mpya wa masomo 2017/18 unaotarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu.

Kabla ya mabadiliko hayo, udahili huo ulikuwa ukifanywa na TCU kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) kwa wale wa stashahada.

Mfumo huu umekuwapo kwa muda mrefu kabla ya kubadilishwa, ambapo sasa udahili utafanywa na vyuo vyenyewe kisha kuwasilisha majina ya wanafunzi waliodahiliwa kwa tume hiyo.

Kubadilishwa kwa mfumo huu kunaelezwa kuchagizwa na mambo mengi ikiwamo kasoro za mara kwa mara ambazo zilikuwa zikijitokeza ikiwa ni pamoja na wanafunzi kupangiwa vyuo wasivyoomba.

Kadhalika kulikuwa na malalamiko ya kudahiliwa kwa wanafunzi wasio na sifa za kusoma elimu ya juu licha ya kutokuwa na sifa zinazowaruhusu kupata elimu hiyo.

Ni ukweli usiopingika kwamba TCU ilizidiwa na mzigo wa wanafunzi kutokana na idadi yao kuwa kubwa ikilinganishwa na uwezo wao na muda wa kupitia sifa za wale wanaoomba nafasi.

Bila shaka mfumo huu mpya utatatua changamoto na kasoro zote zilizokuwapo kabla na kufungua ukurasa mpya wa utendaji wa tume kwani vyuo vimepewa jukumu la kuchagua aina ya wanafunzi wenye sifa wanazozihitaji bila kupangiwa na yeyote.

Zaidi mfumo huu unatoa nafasi ya wanafunzi kuomba vyuo wanavyomudu gharama zake kulingana na uwezo wao kifedha hivyo kutoa unafuu hata kama watoksa fursa ya kupata mikopo.

Wanafunzi watakuwa wamedahiliwa na vyuo vyenyewe hivyo naamini haitakuwa kazi ngumu kwa tume kuwahakiki kwani itakuwa katika nafasi bora zaidi ya kufanya hivyo hata kama masomo yatakuwa yameanza.

Ni wazi kuwa vyuo vitajitahidi kudahili wanafunzi wenye sifa ili kuepuka kashfa ya kuwa na vihio ambao wanaweza kuharibu sifa yao.

Mfumo huu umebeba matumaini makubwa kwa mustakabali wa elimu yetu kwa kipindi hiki ambacho Serikali inapigana kuhakikisha inatoa elimu bora inayoendana na mabadiliko ya kiuchumu, sayansi na teknolojia.

Ikiwa lengo la mfumo huu ni kuleta mabadiliko basi vyuo vinapaswa kuonesha weledi wa wataalamu walionao wakati wa udahili ili kuepuka kasoro ambazo kabla ziliekezwa kwa TCU.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles