26.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Vyeti vya wanafunzi Sekondari Kibara vyadaiwa kuuzwa

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

VYETI vya wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na cha sita mwaka 2016 Shule ya Sekondari Kibara mkoani Mara, vinadaiwa kuuzwa kwa watu wasiojulikana, hivyo kuwafanya kukosa vyeti halali vya kuhitimu masomo yao.

Katika uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, imebainika kuwa wanafunzi waliomaliza shuleni hapo hawajapata vyeti vyao na kwamba taarifa zisizo rasmi zinaeleza vimeuzwa, lakini uongozi wa shule hiyo unaeleza vimepotea.

Katika mahojiano kwa njia ya simu jana na Mkurugenzi wa shule hiyo, Maige Mugeta, alisema ni kweli vyeti hivyo vimepotea, lakini hawezi kutoa maelezo kuhusu namna vilivyopotea.

Alisema si jukumu la mwandishi wa habari kujua kuwa vyeti hivyo vilipoteaje, kwa kuwa yeye si chombo cha usalama, hivyo hana mamlaka ya kuhoji kuhusu upotevu huo au namna vilivyopotea.

“Ninavyojua mimi hivi vyeti ni nyaraka za Serikali, kwa hiyo unapotokea upotevu tunachotakiwa ni kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama, kitakachofuata ni kwa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) kujua nini cha kufanya,” alisema.

Alieleza kuwa kwa kuwa cheti huwa hakitolewi mara mbili, baada ya Necta kupata taarifa, watatakiwa kutoa ‘Hati ya Matokeo’ kuwatambulisha wanafunzi waliopotelewa na vyeti hivyo katika taasisi zitakazokuwa zikihitaji kujua uhalali wa vyeti vyao.

Alipoulizwa idadi ya vyeti vilivyopotea, alijibu: “Wewe kazi yako ni kuweka taarifa kwenye gazeti. Suala la idadi au vimepoteaje inakuhusu nini? Wewe toa hiyo taarifa kwanza huenda ikasaidia. Sema tu vyeti vya shule fulani vimepotea, tutangazie, kwaheri,” alisema kisha akakata simu.

Mmoja wa wazazi wa wanafunzi aliyezungumza na MTANZANIA (jina linahifadhiwa), alisema walibaini kuwa vyeti hivyo havipo baada ya kuvifuata ili kuwasajili watoto wao vyuoni na kufuatilia taratibu za kupata mikopo ya elimu ya juu.

Alisema kwa pamoja walipojaribu kufuatilia hawapewi majibu yanayoeleweka, lakini vyanzo vyao ndani ya shule hiyo viliwaarifu kuwa si rahisi kuvipata kwa kuwa kuna ‘mchezo mchafu’ unaoendelea miongoni mwa viongozi wa shule hiyo.

“Wazazi tulijitahidi kufuatilia, hatujapata vyeti wala hatujapewa utaratibu unaoeleweka wa kupata vyeti vyetu, zaidi tunapewa taarifa ya polisi (RB), tunaambiwa tufuatilie, sasa tutafuatilia wapi?

“Vyeti hivi havijapotelea mikononi mwetu, vimepotelea shuleni, sasa sisi tutaanzia wapi kufuatilia? Uongozi wa shule ndio unaotakiwa kufuatilia na kutupa majibu sahihi yenye suluhisho,” alisema.

Alisema kwa pamoja wazazi wa wanafunzi hao waliamua kujiandikisha ili kujua idadi yao na hadi kufikia jana tayari 17 walishajitokeza wakilalamika kuwa vyeti vya watoto wao havipo.

MKUU WA SHULE

Mkuu wa shule hiyo, Janeth Joseph, alisema ni kweli kuna taarifa kuwa vyeti hivyo vimepotea, lakini yeye bado hajajua mazingira ya kupotea kwake.

Alisema yeye aliingia shuleni hapo Februari mwaka huu na kupokea ofisi, na alikuta RB ya Polisi kuhusu kupotea kwa vyeti hivyo na kwamba tangu wakati huo amekuwa akipokea wanafunzi wanaofuata vyeti vyao.

“Vyeti vilivyopotea ni vya mwaka 2016 pekee, vyeti vya miaka mingine, yaani 2017 vipo na vya mwaka 2015 vipo, lakini vya 2016 havipo.

“Sasa kuhusu upotevu huo, huenda mmiliki wa shule au mkurugenzi ndio wanaoweza kutoa maelezo ya kina kwa kuwa watakuwa na taarifa nzuri kutoka kwa wakuu wa shule waliopita,” alisema.

MENEJA WA SHULE

Meneja wa shule hiyo, Andrew Wabiae, alisema hana taarifa kamili kuhusu namna vyeti hivyo vilivyopotea ila wanaoweza kuzungumzia suala hilo ni mkuu wa shule au mkurugenzi.

Wabiae alisema kwa taarifa za haraka alizonazo ni kwamba vyeti vya waliohitimu shuleni hapo kwa mwaka juzi vyote bado viko kwenye ofisi ya Ofisa Elimu Wilaya ya Bunda na havijakabidhiwa kwa shule.

Alisema vyeti hivyo havijakabidhiwa shuleni kwa kuwa kuna matatizo kidogo yalijitokeza, hivyo kuchelewesha hatua ya kuvikabidhi.

Alipoulizwa kuhusu matatizo hayo yaliyosababisha vyeti hivyo kutowasilishwa shuleni hadi sasa, alisema hawezi kuyazungunzia kwa kuwa mkurugenzi ndiye anayejua kila kitu.

Alieleza kuwa kwake yeye, ana taarifa kwamba vyeti vya waliohitimu kidato cha nne na cha sita mwaka 2016 ndivyo havionekani kabisa shuleni hapo, lakini hakuna taarifa kuwa vimekwenda wapi.

“Kwa hiyo tunaendelea na utaratibu wa kuchukua hatua, kwa wanaokuja kama wanahitaji vyeti na ni lazima, tunawapa taarifa ya polisi kuhusu upotevu wa vyeti vyao ili waendelee kufuatilia maeneo mengine,” alisema.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu iwapo uamuzi wa kuwapa taarifa ya polisi wanafunzi kufuatilia vyeti vyao inamaanisha kuwa vimepotelea shuleni hapo, alisema yuko katika kikao na hawezi kujibu hilo kwa sasa, kwa kuwa maelezo zaidi yako kwa mkurugenzi, kisha akakata simu.

OFISA ELIMU

Ofisa Elimu ya Sekondari Wilaya ya Bunnda, Sylvester Mrimi, alisema anafuatilia suala hilo, ila kwa sasa mwenye uwezo wa kulizungumzia kwa undani ni mkurugenzi wa shule hiyo, Mugeta.

Alisema suala hilo liko mikononi mwa uongozi wa shule na Necta, na kwamba ofisi yake itaendelea kufuatilia taarifa hizo kujua ukweli, kwa kuwa shule hiyo iko katika eneo lake.

“Uongozi wa shule ndio wenye majibu yote kuhusu suala hilo. Ila ofisi yangu pia itafuatilia suala hili kujua liko vipi kwa sababu bila kupata taarifa sahihi hatuwezi kuingilia mambo yaliyoko chini ya uongozi wa shule, zaidi vyombo vya usalama ndivyo vinavyotakiwa kushirikishwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles