25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

‘VYETI FEKI VYATIKISA UHAI WA TALGWU’

Na MASYENENE DAMIAN -MWANZA

CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa(TALGWU)kimesema hatua ya Serikali ya kutafuta wafanyakazi hewa, wenye vyeti vya kughushi na wenye elimu ya darasa la saba, ilikitikisa chama hicho na kutishia uhai wake.

Hayo yamebainishwa katika mkutano wa nusu mwaka wa wenyeviti wa mikoa wa chama hicho uliofanyika jijini Mwanza jana.

Mwenyekiti wa TALGWU,Selemani Kikingo, alisema kwa kipindi cha nusu ya mwaka huu, chama hicho kimepitia changamoto nyingi zilizoathiri maendeleo yake na kutishia uimara wake, hivyo kuwataka wenyeviti wa mikoa kukiimarisha kwa kusajili wanachama wapya.

“Sakata la wafanyakazi hewa, vyeti vya kughushi na watumishi wa darasa la saba, kama tusingekuwa na nguvu katika usajili wa wanachama, tungefika mahali tukashindwa kujiendesha… kipindi hiki cha miezi sita tumekumbwa na mtafaruku, wanachama wetu 2,744 walikuwa wahanga wa tatizo la watumishi hewa.

“Tumeendelea kukutana na TUCTA (Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi) na Serikali kuona namna ya kupata suluhu ya tatizo hilo na kufikia makubaliano, hivyo nawaomba viongozi na wanachama waliokumbwa na hilo tatizo kuendelea kuvuta subira wakati unatafutwa ufumbuzi.

“Tunaendelea kukusanya taarifa kwa sababu yapo maeneo ambayo yanaonyesha yana utata, tunaendelea kujiridhisha na itabidi twende kwenye vyombo vya sheria kuhakikisha sheria zinatafsiriwa, hasa sheria za ajira zilizotumika kuwaondoa kazini… tusisite, tusirudi nyuma tuendelee kutetea haki zetu bila kuvunja sheria,” alisema.

Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, Rashid Mtima, alisema licha ya kupitia kipindi kigumu, wataendelea kukusanya taarifa za wanachama wao wanaohusika na sakata la kutofikia elimu ya sekondari.

Alisema ipo haja ya kutafuta tafsiri ya kisheria ya namna mambo yalivyofanyika kwa Serikali kuwaondoa watumishi hao serikalini bila kuzungumza na chama chao.

Kwa upande wake, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, alisema shirikisho hilo linaendelea kufanya majadiliano na Serikali namna ya kuwalipa stahiki zao watumishi walioondolewa kazini na kushughulikia rufaa zao.

“Hatuko nyuma, tunaendelea kupigania maslahi ya wafanyakazi na naamini yote yatapatiwa ufumbuzi hivi karibuni, wiki hii tutakutana na makatibu wakuu wa Wizara ya Kazi na Ajira, matatizo ya watumishi tutayatatua, kwa wale wa darasa la saba wengine tayari wamerudishwa kazini,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles