Patricia Kimelemeta na Grace Shitundu
OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imevitaka vyama vya siasa vilivyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, kuwasilisha ripoti ya matumizi ya fedha zilizotumika wakati wa kampeni, kulingana na matakwa ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi.
Sheria hiyo imeweka viwango vya matumizi ya fedha, ambapo nafasi ya urais ni Sh bilioni 15, ubunge ni Sh milioni 33 hadi milioni 88 kulingana na jografia ya jimbo, huku nafasi ya udiwani ikiwa ni Sh milioni 2 hadi milioni 7.
Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza, alisema chama kilichoshindwa kuzingatia mwongozo wa sheria hiyo na kuzidisha kiwango kilichopangwa (over budget), kitachukuliwa hatua.
Nyahoza alisema chama kilichokiuka sheria hiyo kitalazimika kulipa faini ya Sh milioni tatu ikiwa ni adhabu ya nyongeza, kutoshiriki uchaguzi mdogo utakaojitokeza kati kati pamoja na Uchaguzi Mkuu wa 2020.
“Mgombea bila ya kujali kama ameshinda au ameshindwa kwenye uchaguzi, ikiwa atashindwa kuandaa ripoti iliyoelekezwa katika kifungu kidogo(1) ametenda kosa na kwamba akibainika anatakiwa kulipa faini isiyozidi Sh milioni 2 au kifungo cha mwaka mmoja au adhabu zote kwa pamoja,”alisema Nyahoza.
Alisema kwa upande wa wabunge, gharama za matumizi ya fedha zimegawanyika katika makundi sita kutokana na ukubwa wa jimbo, idadi ya watu na ubora wa miundombinu ya mawasiliano.
Alisema katika sheria hiyo inawataka wagombea wa kundi la kwanza kutumia Sh miloni 33, wakati kundi la pili wanatumia Sh milioni 44, huku kundi la tatu wakitumia Sh milioni 55.
“Kundi la nne wanatakiwa kutumia Sh milioni 66 na kundi la tano kutumia Sh milioni 77 na kundi la sita na la mwisho wanatakiwa kutumia Sh milioni 88, hivyo basi kila mgombea anajua ameingia kwenye kundi gani kulingana jimbo lake,”alisema.
Akizungumzia upande wa viti maalumu, Nyahoza alisema kuwa, wagombea hao wanatakiwa kutumia kiasi cha juu cha fedha cha Sh milioni 10.
Alisema madiwani wa meneo ya mijini wanatakiwa kutumia Sh milioni 7 na wa maeneo ya vijijini wanatakiwa kutumia Sh milioni 5.