Na ANDREW MSECHU
VIONGOZI wa vyama 10 vya siasa wameipongeza Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa busara ya kuwaita, kuwasikiliza na kuchukua maoni yao na kuyafanyia kazi, huku vikiiomba iendeela kutumia busara ya kuyafanyia kazi mapendekezo kuhusu maeneo ambayo bado hayajafanyiwa kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kwa niaba ya viongozi wa vyama vyote jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema Kamati ya Bunge imeshafanya kazi yake lakini ni vema iendelee kurekebisha na kupokea mambo mengine.
Pia aliliomba Bunge liendelee kufanya mabadiliko ilipoishia kamati hiyo ili kutengeneza mazingira ya siasa inayosimamia demokrasia.
Alisema ingawa kamati imepunguza adhabu ya makosa kutoka Sh milioni moja hadi Sh 500,000 na kupunguza kifungo kutoka miezi sita hadi mitatu, ipo haja ya kuondoa masuala ya kuifanya siasa kuwa jinai.
Alisema zipo sheria zinazosimamia makosa ya jinai ambayo yanaingizwa katika namabadiliko hayo, ambazo zitaweza kutumika kwa wote watakaokiuka sheria ndani ya vyama.
“Katika maoni tuliyoyatoa kwenye kamati Januari 19 na 20, mwaka huu mjini Dodoma, tulipinga muswada huo wa mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa wenye ukakasi kwa kuieleza kamati hiyo umuhimu wa kutumia uhuru na mamlaka yake ya katiba kulisaidia taifa hasa katika muswada huo wenye nia ya kumpa mamlaka makubwa msajili wa vyama vya siasa.
“Tuliwaeleza siasa inajenga taswira na sura ya taifa kwenye macho ya dunia na kwamba siasa inahusisha vyama vya siasa ambavyo ndiyo wadau wakuu wa siasa katika nchi.
“Hivyo kutunga sheria inayovifanya vyama vya siasa kutokuwa huru ni kutengeneza taswira mbovu ya nchi mbele ya sura ya dunia,” alisema.
Alisema watu wanapokosa fursa katika siasa na kukosa kuona inaweza kubadili maisha yao na kutimiza ndoto zao, unawasukuma kuangalia njia nyngine nje ya siasa na kuanza kuleta mambo mengine yasiyo ya ustaarabu na hivyo kuleta athari kubwa ndani ya taifa.
“Bahati nzuri baada ya sisi kuwasilisha maoni yetu, Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria imepitia mawazo ya wadau na namna ilivyoyachambua, na baadhi yamechukuliwa, baadhi yameachwa na mengine yameongezwa na kamati yenyewe,” alisema.
Alisema katika suala la mafunzo ya uraia na kujenga uwezo, walijenga hoja na kamati baada ya kupitia mapendelezo imeona umuhimu wa kumwekea msajili vigezo vya kusema aina gani ya maombi ya mafunzo atayakubali au atayakataa tofauti na awali ambako mapendekezo hayakuwa na muongozo wowote wa namna ya kuyakubali au kuyakataa.
Alisema ingawa halijakamilika kwa silimia 100 lakini wamekutana nusu ya njia suala ambalo bado wanaendeela kuiomba Kamati kuliangalia kwa undani zaidi kwa kuwa suala la kujenga uwezo ni zaidi ya elimu ya uraia hivyo hakuna sababu ya msajili kuingilia hilo na kuona namna ya kutenganisha elimu ya uraia na suala la kujenga uwezo.
“Suala jingine ni kumpa uwezo msajili kuomba taarifa kutoka kwa chama, kiongozi au mwanachama yeyote.
“Kamati imeelewa na kuondoa kipengele cha mwanachama au kiongozi yeyote na kuweka kiongozi wa chama.
“Lakini ni vema kuainisha kwamba taarifa zote lazima ziombwe kwa Katibu Mkuu wa chama kwa kuwa ndiye msimamizi wa taarifa zote za chama,” alisema.
Alisema suala jingine ni kuondoa kinga ya kushtakiwa kwa msajili, naibu wake na maofisa wote ila kwa jambo alilofanya kwa nia njema na kurudisha uwezekano wa msajili kushtakiwa kwa jambo alilolofanya kwa uzembe.
Alisema sura ya sita na saba ya sheria hiyo ilitaka chama kisiwe cha uanaharakani ambako walitaka tafsiri ya uanaharakati kwa kuzingatia chama chochote cha siasa kiko kwa ajili ya kutetea jamii.
Alisema sura hiyo ililenga kuviziba mdomo vyama hivyo lakini kamati imeona ni vema kuondoa kipengele hicho.
Mwalimu alieleza kuwa suala jingine ni kuondolewa kipengele kilichokuwa kikilazimisha mtu kuruhusiwa kusajili chama baada ya kuthibitishwa uraia wake na wa wazazi wake.
Alisema kipengele hicho kinapingana na Katiba inayomtaka mtu kuwa raia wa Tanzania bila kujali uraia wa baba au mama kuchaguliwa na pia suala la umri wa miaka 21 ili kuanzisha chama wakati katiba inataka miaka 18 hivyo Kamati iliondoa na kutruhusu umri wa kuanzisha chama kuwa miaka 18.
“Muswada huu ulikuwa unampa waziri mamlaka ya kutunga kanuni kusimamia ushirikiano wa vyama wakati akiwa mteule wa rais anayetokana na chama.
“Sasa mtu kutoka chama X anawezaje kuja kututungia vyama vingine kanuni? Tulilalamikia suala hili na kipengele hiki kimeondolewa na Serikali imetakiwa kutengeneza jedwali kuonyesha namna ya muungano wa vyama kabla na baada ya uchaguzi,” alisema.
Alisema pia suala la msajili kuzuia ruzuku limeondolewa ila msajili ataruhusiwa kuzuia ruzuku iwapo tu kuna tatizo la msingi na atazuia kwa kipindi maalumu.
“Pia kwa kuwa hana mamlaka ya ueledi ya kubaini hesabu na kusimamia suala la bajeti, kamati imesikia kilio chao na kuelekeza msajaili atazuia tu ruzuku kutokana na ripoti ya CAG.
Mambo yaliyoachwa
Alisema mambo ambayo bado yanahitaji kufanyiwa mabadiliko ni suala la majukumu ya msajili kwenye uchaguzi wa ndani ya vyama.
Walipendekeza asihusike moja kwa moja bali awe mwangalizi na asiwe sehemu ya mchakato bali awe mshauri anayeweza kupokea malalamiko na kurekebisha kasoro kuliko kuwa sehemu ya uchaguzi hoo, hivyo wametoa ombi kwa kamati hiyo kuliangalia kwa kina suala hilo na kulifanyia kazi.
Alisema ni wazi kwamba kwa sasa msajili amekuwa chanzo cha kupandikiza migogoro kwenye vyama vikiwamo DP na CUF na hivyo ni vema kamati ione umuhimu wa kumuondolea msajili mamlaka hayo na kumfanya awe mwangalizi.
Alisema suala jingine ni kuzuiwa kukasimishwa madaraka ya mkutano mkuu kwa kamati za uongozi suala ambalo hufanyika kwa taratibu za ndani za vyama hasa wakati mwingine kutokana na udharura wa mambo na uwezekano wa kukutana kwa haraka, suala ambalo hufanyika kwa taarifa za kina na kwa maridhiano kutokana na ustaarabu wa uongozi.
Alisema kuhusu Tunu za Taifa suala hilo limeachwa vile vile ingawa wamekuwa wakilalamikia mambo mawili ambayo ni lile linalosema Tunu za Taifa ni pamoja na Mwenge ambao umekuwa ukitumiwa na CCM kwa faida yao, hivyo jambo linalotekelezwa na chama kimoja haliwezi kuwa tunu ya taifa, labda lirudishwe kwenye misingi ya taifa.
Alisema suala jingine ni kutaja Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano kuwa ni Tunu ya Taifa na kuacha suala la Uhuru wa Tanganyika.
Kwa sababu hiyo wanaendelea kupendekeza iwapo wanashindwa kuweka suala la uhuru wa Tannganyika basi ni vema suala la mapinduzi liondolewe na libaki suala la Muungano pekee kwa kuwa ndiyo unaohusisha pande zote mbili.
Alisema suala jingine ambalo halijarekebishwa ni kutaka kuondoa utaratibu wa vyama kujilinda kwa kutaka kuondoa walinzi wa viongozi wa vyama na mali za vyama wakati wanajua kwamba hakuna polisi wanaoweza kuwalinda viongozi wala mali za vyama.
Alisema siyo sahihi kuwa kuna vikundi vya jeshi au vya ugaidi bali kuna vikundi vya ulinzi wa viongozi na mali za vyama.