27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

Vurugu Afrika Kusini zavuka mipaka

jacob-zumaDurban, Afrika Kusini

LICHA ya Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma kulaani vurugu zinazoendelea nchini humo dhidi ya wageni (xenophobia), vurugu hizo zimezidi kupamba moto na sasa zimevuka mipaka ya nchi hiyo.
Wakati vurugu zikiendelea kwa wenyeji kuvamia na kuiba kwenye maduka ya raia wa kigeni katika hali ambayo imeonesha kama ni kulipa kisasi, raia wa Afrika Kusini wanaoishi na kufanya biashara katika nchi za Msumbiji na Zimbabwe siku nzima ya jana baadhi yao wameanza kushambuliwa.
Taarifa hizo zilisema nchini Msumbiji raia wa nchi hiyo walikuwa wakiyashambulia maroli yenye namba za usajili za Afrika Kusini.
Pia kutoka nchini Zimbabwe, taarifa zilieleza kuwa leo wanafunzi wa vyuo vikuu vyote vya Zimbambe wanaandamana kwa nia ya kufanya fujo kwenye biashara za wawekezaji waliopo hapo.
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya, aliliambia gazeti hili kuwa hakuna Mtanzania hata mmoja aliyeathirika na vurugu hizo.
Alisema zipo taarifa kuwa kuna Watanzania wawili waliofariki vifo vya kawaida mmoja kutokana na kuugua kwa muda wa miezi miwili na mwingine kutokana na kuchomwa kisu akiwa gerezani.
Hata hivyo, chanzo cha kuaminika nchini humo kinasema kuna Watanzania wengi wanaoishi Durban kama wahamiaji haramu na huenda wameathirika kwa namna tofauti.
Mmoja wa Watanzania anayeishi karibu na mpaka wa Afrika Kusini na Msumbiji ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema zaidi ya malori 100 yanayosafirisha makaa ya mawe yanayozalishwa Mpumalang’a yamekwama baada ya mpaka huo kufungwa juzi.
“Leo hakuna lori lililopita, tunaambiwa kuna msururu wa malori umbali wa maili tatu hivi. Wenyeji wangu wametuma mabasi kuja kuchukua ndugu zao. Hali si nzuri, wenzetu wanajua kulipiza kisasi bila kupiga mayowe,” alisema.
Vurugu zilivyoanza
Kwa mujibu wa mtandao wa BBC, kundi la watu lilianza kuvamia maduka ya wageni Mashariki ya Johannesburg Alihamisi wiki iliyopita. Zaidi ya wageni 200 walikimbilia kwenye kituo cha polisi na ililazimu kutumika mabomu ya machozi kuwatawanya wavamizi na kukamata watu 12.
Mmoja wa mashuhuda alisema kundi la watu lilishushwa kwenye basi dogo na wote walikuwa wamebeba silaha kama visu na mapanga na walianza kuwafukuza watu hovyo.
Ijumaa, polisi walitumia risasi za mpira kutimua kundi la washambuliaji waliokuwa wamesheheni mapanga.
Kaimu kiongozi wa Jimbo la Gauteng, jijini Johannesburg, Qedani Mahlangu aliwataka Waafrika Kusini wanaoipenda nchi yao kupinga uvamizi huo.
Takwimu zinaonyesha kuna wageni wapatao milioni mbili Afrika Kusini sawa na asilimia nne ya idadi ya watu wote, lakini wengine wanakadiriwa kuwa wanafikia milioni tano.
Katika Jimbo la Gauteng linalohusisha Johannesburg, asilimia saba ya idadi ya watu si raia wa nchi hiyo.
Mwaka 2012, asilimia 17 ya Wazimbabwe walipata vibali vya muda vya kuishi nchini humo wakifuatiwa na wananchi kutoka nchi za Nigeria, India, China, Pakistan na Uingereza.
Mfalme wa kabila la Wazulu, Goodwill Zwelithini, anatuhumiwa kwa kuchochea mashambulio hayo aliposema kuwa wageni wanapaswa kuondoka na kurudi kwenye nchi zao. Japo amesema ameshaifuta kauli hiyo.
Polisi wameanzisha kambi za muda zinazofanya kazi saa 24 ili kutuliza ghasia. Waafrika Kusini wengi hawapendi fujo hizo, lakini hawafurahii kiwango cha wahamiaji wanaomiminika nchini kwao wakiamini kuwa wageni hao wanazidi kuwafukarisha.
Wahamiaji wengi kutoka nchi za Afrika na Asia wamekuwa nchini humo kwa wingi tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1994. Waafrika Kusini wanawalalamikia kwa kuchukua kazi zao wakati kiwango cha ukosefu wa ajira kikiwa ni asilimia 24.
Watu 68 waliuawa kwenye mashambulio kama hayo yaliyotokea mwaka 2008.
Yasemavyo magazeti ya Afrika
Baadhi ya magazeti barani Afrika yametoa maoni kutokana na vurugu hizo. Gazeti la Newsday la Zimbabwe limesema: “Zimbabwe inapaswa kurejesha uchumi wake kuwa imara ili raia wake wasiendelee kuwindwa kama wanyama katika ardhi ya ugenini. Ubaguzi siyo aibu tu kwa Afrika Kusini bali kwa bara zima.”
Gazeti la Nyasa Times limeandika: “Tukiwa kama Wamalawi, hebu tuwe na msimamo wa pamoja wa kuonyesha hasira. Kwa kuanza, hebu tugomee biashara za Waafrika Kusini.”
Gazeti la L’Observateur la Burkina Faso limeandika: “Kitu cha kutisha zaidi ni kwamba, yote yanayotokea Afrika Kusini hayana tofauti na utawala wa nchi hiyo. Imechukua siku kadhaa kwa kuchelewa tangu vurugu zilipoanza Durban hadi rais wao alipotoa tamko.”
Hivi karibuni wananchi wapatao 5,000 waliandamana kupinga vurugu hizo, lakini maandamano hayo hayajasaidia kitu. Tukio jipya lilitokea Mashariki mwa Jiji la Johannesburg. Tayari watu watano wamekufa tangu vurugu hizo zilipoanza wiki chache zilizopita.
Polisi wamelazimika kuweka mpaka wa magari yao kwenye maduka ya wageni dhidi ya wananchi wenye hasira.
Akizungumza katika bunge la nchi hiyo, Rais Zuma alisema vurugu hizo zimeleta mshtuko mkubwa.
“Hakuna kiwango cha hasira au kuchanganyikiwa kunakohalalisha mashambulizi dhidi ya wageni na kuiba kwenye maduka yao,” alisema Zuma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles