25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Viziwi wawezeshwa kufanya kazi kwa usalama

Na Mwandishi Wetu

KUFUATIA mchango wa watu wenye ulemavu katika shughuli za uzalishaji nchini, Serikali imesema kuna umuhimu wa kuwawezesha kupitia mafunzo ya usalama na afya kazini pamoja na kuwapa mitaji ili wawaze kuboresha shughuli zao za kiuchumi.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika, kwenye ufunguzi wa mafunzo ya kukuza uelewa wa masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha) kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (Tamavita) Mkoa wa Mbeya.

Mafunzo hayo ya siku moja yalijikita katika kuainisha na kushauri mbinu mahsusi za kudhibiti vihatarishi vya usalama na afya ambavyo huambatana na shughuli mbali mbali za uzalishaji ikiwemo ujenzi, kilimo, useremala, kilimo, ufugaji, biashara ndogo ndogo pamoja na kazi za maofisini.

Miongoni mwa vihatarishi vilivyoainishwa na watalaam wa Osha katika mafunzo hayo ni pamoja na  vumbi, kelele, kemikali, umeme, mitambo na zana mbali mbali za kazi.

 “Pamoja na Serikali kutenga fungu maalum la fedha kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa makundi mbali mbali katika jamii ambapo asilimia mbili ya fedha hizo ni kwa ajili ya watu wenye ulemavu, kama Serikali tunaona kuna umuhimu wa kutoa mafunzo ya usalama na afya kwa makundi lengwa ili waweze kuepuka madhara yanaweza kusababishwa na kutozingatia kanuni za usalama na afya kazini,” Ntinika.

Aliipongeza Osha kwa kutekeleza ipasavyo wajibu wake ikiwemo kufanya kaguzi za usalama na afya katika sehemu nyingi za kazi pamoja na kuwaelimisha wananchi kuhusiana na masuala ya afya na usalama kazini na kuitaka kuongeza jitihada zaidi ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alisema mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa kwa makundi mbali mbali ya kijamii wakiwemo watu wenye ulemavu katika mikoa mbali mbali na kusisitiza kwamba mafunzo hayo ni endelevu.

“Kama taasisi yenye dhamana ya usalama na afya kwa mfanyakazi, tumeona kuna umuhimu wa kuyafikia makundi haya ya watu wenye ulemavu kwakuwa tunatambua kwamba ulemavu ni hali tu na haupaswi kuwa kikwazo kwa mtu kushiriki katika shughuli kiuzalishaji. 

“Tumeshayafikia makundi mbali mbali ya watu wenye ulemavu katika mikoa kadhaa ikiwemo Kagera, Dar es Salaam, Pwani na sasa Mbeya na tutaendelea kutoa mafunzo haya katika mikoa mingine,” alisema.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Renatha Exsavery ambaye ni mwanafunzi wa ufundi katika Chuo cha VETA Mbeya na Queen Majembe, walieleza kufurahishwa kwao na mafunzo waliyoyapata ambapo wamesema mafunzo hayo yatawawezesha kujilinda dhidi ya vihatarishi mbali mbali vilivyopo katika sehemu zao za kazi.

“Mafunzo haya tuliyoyapata leo tumeyaona yanafaida nyingi kwani yatatusaidia kulinda afya zetu na kupitia mafunzo haya tutakuwa waangalifu zaidi katika kazi mbali mbali ambazo ni hatarishi hususan kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa kinga muhimu,” alisema Renatha Exsavery, Mshiriki wa Mafunzo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles